Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
MASHEIKH na viongozi wa dini ya kiislamu Wilaya ya Ubungo wamefunguka jinsi wanavyovutiwa na utendaji kazi wa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo kutokana na ukaribu wake na wananchi.
Viongozi hao wa dini wamebainisha hayo Aprili 16, 2023 wakati wa hafla ya Iftari iliyondaliwa na mbunge huyo kwenye hoteli ya Lion iliyopo Sinza, Dar es Saalam.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakiongozwa na Shekhe wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Kidebe, walisema licha ya kuwa mbunge, Profesa Kitila amekuwa mnyenyekevu kwa kila mtu.
“Tunampenda sana mbunge wetu Profesa Kitila Mkumbo kwa sababu ni mbunge mnyenyekevu katika jamii yote inayomzunguka bila kujali dini,” amesema Sheikh Kidebe.
Naye Mjumbe wa Baraza la Masheikh Wilaya ya Ubungo, Ramadhan Maneno amesema wanafurahi kupata mbunge wa aina hiyo anayemjali kila mmoja, huku akimshikuru kwa kufanya ibada hiyo ya kufuturisha.
“Nimpongeze mbunge wetu Kitila Mkumbo kwa jambo kubwa alilolifanya akitambua nini kinaendelea katika mwezi huu licha ya kwamba yeye sio wa imani hii, tunashukuru na tupo pamoja kuhakikisha Wilaya yetu ya Ubungo inapata maendeleo,” amesema diwani wa Msigani Hassan Mwasha kwa niaba ya madiwani wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake Profesa Kitila, amewashukuru viongozi hao kwa kuendelea kumuunga mkono na kuwaomba wazidi kumuombea ili atimize majukumu yake na asibadilike bali azidi kuwa mnyenyekevu.
“Nimekuwa na utamaduni wa kufanya jambo hili kila mwaka, lengo ni kujumuika pamoja na kutekeleza ibada hii. Naomba muendelee kuniombea, pia kumuombea Rais Samia ili nchi iendelee kuwa na amani,” amesema mbunge huyo.