THE HAGUE, UHOLANZI
WAENDESHA Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, wamekubali ombi la kuachiwa huru rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, lakini kwa sharti kwamba asirejee katika nchi yake kama anavyotaka.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Helen Brady amewaambia majaji kuwa, wana wasiwasi kwamba huenda Gbabgo na mpambe wake, Charles Ble Goude wasirejee katika mahakama hiyo iwapo majaji wa ICC watatoa uamuzi wa kusikilizwa upya kesi zao.
Hata hivyo, wakili wa Gbagbo, Emmanuel Altit, anasisitiza kuwa mteja wake anapaswa kuachiwa huru mara moja bila masharti yoyote na aruhusiwe kurejea nchini kwake haraka iwezekanavyo.
Waendesha Mashitaka wa Mahakama ya ICC ambao walikata rufaa kupinga uamuzi wa wawili hao kuachiwa huru, wanataka waachiwe huru na kisha wapelekwa katika nchi jirani na Uholanzi, sambamba na kutwaliwa pasi zao za kusafiria.
Mwezi uliopita, ICC ilifuta mashtaka na kuwaachilia huru Gbabgo pamoja na mpambe wake, Charles Ble Goude, ambao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kuhusika katika ghasia baada ya uchaguzi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Wawili hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai dhidi ya binadamu katika mwaka 2010 na 2011 katika vita ya ndani nchini mwao ambako watu 3,000 waliuawa.