Na AGATHA CHARLES
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimewateua mbunge wa zamani wa Jimbo la Nyamagana, Ezekiel Wenje na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, kugombea nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki (EALA).
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema jana kuwa majina hayo yalipitishwa na kikao cha Kamati Kuu Maalumu kilichoketi Machi 22 na 23, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
“Kikao kilikuwa na ajenda mbili na hii ilikuwa mojawapo. Kamati Kuu ilipata kuwasikiliza wagombea na baada ya tafakari nzito ya siku mbili, iliwateua Wenje na Masha kuwa ndio wagombea wawili watakaopeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki.”
Alisema wagombea wataendelea na taratibu nyingine kwa mujibu wa tangazo na kanuni za kibunge.
Mnyika ambaye alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye alipata dharura ya shughuli za kichama mkoani Tanga ambako pia ataendelea na ziara mikoa ya Kanda ya Kaskazini, alisema uamuzi huo umekuja kutokana na uchaguzi wa wabunge wa EALA kutarajia kufanyika Bunge lijalo la mwezi Aprili.
Mnyika alisema Bunge hilo linawakilishwa na wabunge tisa kutoka nchini na wao Chadema wana nafasi mbili, CCM sita huku CUF wakitakiwa nafasi moja.
Hadi sasa ni Chadema pekee ambacho kimetangaza majina ya wagombea wake huku gazeti moja la kila siku likiripoti juzi kuwa wagombea 300 kutoka bara na visiwani walichukua fomu kuwania nafasi hizo kupitia CCM.
Uchaguzi huo wa wabunge wa EALA utafanyika Aprili 4, mwaka huu kwa kuchagua wabunge tisa wa kuiwakilisha Tanzania katika Bunge hilo lenye makao yake makuu jijini Arusha.