Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Serikali imesema ni marufuku mwanafunzi yeyote kujiunga na shule ya bweni bila kupimwa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa agizo hilo leo Jumanne Machi 20, wakati akizindua dawa maalumu ya kutibu TB ya watoto.
Aidha, Waziri Ummy amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali kuhakikisha anasimamia suala hilo na kuwapa maelekezo waganga wakuu wa wilaya na mikoa.
Amesema ugonjwa wa TB ni janga duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO), linakadiria kila mwaka zaidi ya watu milioni 10.4 huugua ugonjwa huo na wagonjwa milioni moja kati yao ni watoto wenye umri chini ya miaka 18.
“Takwimu za mwaka 2016 zinakadiria kila mwaka watu 160,000 nchini huugua ugonjwa huo hata hivyo walioweza kugundulika ni takribani watu 65,900 pekee ambao waliingizwa katika mpango wa matibabu.
“Ni changamoto kubwa, yaani kati ya watu 100 wanaogundulika ni watu 40 tu, 60 wote hatuwagundui, wapo majumbani, maofisini, nyumba za ibada na kwingine, ingawa bahati nzuri ni kwamba kati ya watu 100 wanaogundulika na kutibiwa 90 hupona lakini tutawapate ni changamoto,” amesema.
Ummy amesema serikali ilitoa mwongozo kwamba kila mtu lazima ahisiwe kuwa na ugonjwa huu na ikaainisha dalili zake, ambapo walipata matokeo mazuri kwani sasa idadi ya wanaogundulika imeongezeka mara mbili zaidi ya awali.
“Hivyo Mganga Mkuu wa Serikali fuatilia kuhakikisha wanafunzi hawajiungi na shule za boarding bila kupimwa maambukizi ya ugonjwa huu iwapo wanayo au la,” amesema.