WASHINGTON, MAREKANI
SERIKALI ya Marekani imetaka kusitishwa kwa mapigano nchini Yemen na kufanyika mazungumzo ya amani, huku muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ukiyatuma majeshi 10,000 zaidi kuelekea mji wa Hodeida unaodhibitiwa na waasi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis ametaka kuwepo mpango wa kusitisha mapigano nchini Yemen na pande zinazozana kufanya mazungumzo katika kipindi cha siku 30 zijazo.
Mattis alisema Marekani imekuwa ikiutazama mzozo wa Yemen kwa muda wa kutosha na inaamini Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambao ni washirika muhimu wa muungano huo wa kijeshi unaoungwa mkono na Marekani watasitisha mapigano.
Alisema muda umewadia wa kufanya mazungumzo ya kutafuta amani na kuzitaka pande zinazozozana kukutana na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Martin Griffiths nchini Sweden mwezi ujao ili kufikia suluhisho.
Wakati akiutaka muungano huo kusitisha mapigano, pia amewataka waasi wa Houthi kukoma kurusha makombora na kufanya mashambulizi kwa kutumia ndege zisizoendeshwa na rubani dhidi ya Saudi Arabia na UAE.
Zaidi ya watu 10,000 wameuawa katika mzozo huo na wengine milioni 22 ambayo ni theluthi mbili ya Wayemeni wote wakihitaji misaada ya kibinadamu na wengine milioni 8.4 wako katika hatari ya kufa njaa.