WASHINGTON, MAREKANI |
SERIKALI ya Marekani imetangaza kusitisha msaada uliokuwa unatolewa kwa lengo la kuimarisha hali ya maisha ya wananchi wa Palestina, hususan wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.
Taarifa ya Serikali hiyo imetolewa na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje, akisema msaada wa kiasi cha dola milioni 200 kwenda Palestina umefutwa, hatua ambayo imelalamikiwa na Balozi wa Palestina na kuushutumu utawala wa Rais Donald Trump kuwa haupendi amani.
Ofisa Mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema uamuzi huo ulioagizwa na Rais Trump, uliamuliwa baada ya kufanywa tathmini ya programu za usaidizi katika maeneo ya Palestina.
Ofisa huyo ameongeza kwamba, fedha hizo za misaada sasa zitatumika kufadhili miradi yenye umuhimu mahali pengine.
“Tumechukua hatua hii baada ya kufanya tathimini ya misaada ya Marekani kwa Mamlaka ya Palestina, hususan maeneo ya Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, tumeona ni vema fedha hizo zitumike kwenye miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi wa Marekani pamoja na kuheshimu thamani ya kodi yao,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Uhusiano kati ya mamlaka ya Palestina na utawala wa Marekani uliharibika baada ya Trump kutangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
Palestina wanasema mji wa Jerusalem Mashariki ni makao yao kama nchi huru, wakati Israel wamesema mji wa Jerusalem ni makao yao makuu.
Uamuzi huo wa kusitisha msaada wa kifedha kwa Palestina unakuja katika wakati ambao kuna mgogoro mkubwa wa kibinadamu huko Gaza, huku kukiwa na vurugu za maandamano ya mpakani ya kila wiki yaliyoanza Machi.
Wapalestina wapatao 171 wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel, wakati wa maandamano hayo yanayofanyika katika mpaka wa kati ya Palestina na Israel.