MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA mpya wa klabu ya Crystal Palace, Roy Hodgson, amesema ubora wa klabu ya Manchester United ni sawa na bondia mwenye uwezo wa hali ya juu.
Manchester United juzi ilishuka dimbani kwenye Uwanja wa nyumbani wa Old Trafford na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Crystal Palace, hivyo Hodgson amedai hawakuwa na uwezo wa kuwazuia wapinzani hao wasiibuke na ushindi.
Mchezo huo ulikuwa wa saba katika michuano hiyo ya ligi kuu msimu huu, lakini Crystal Palace haikufanikiwa kupata ushindi kwa michezo yote na kuifanya ishike nafasi ya mwisho kwenye msimamo.
Hodgson mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kwenye kazi ya ukocha kwa miaka 40 huku akifundisha jumla ya timu 21 tofuti, alichukua nafasi ya kuifundisha klabu hiyo ya Crystal Palace baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Franke de Boer, kufukuzwa kazi kutokana na kupoteza michezo mitano ya ligi, hivyo Hudgson amekiri kuwa Man United ni habari nyingine.
“Nadhani lazima tukubaliane na matokeo, tulikutana na klabu ambayo ilikuwa kwenye uwezo wa hali ya juu kama bondia, hivyo tulikuwa na kila sababu ya kufungwa katika mchezo huo, siwezi kuwalalamikia wachezaji kwa kuwa hawakuwa na jinsi walizidiwa kila idara.
“Kikubwa ni kujipanga kwa ajili ya michezo inayofuata, ninaamini nitapambana kuhakikisha tunaleta furaha kwa mashabiki na kuondoka kwenye nafasi tuliopo kwa sasa,” alisema Hodgson.
Hata hivyo, kocha huyo anaamini kuwa kikosi chake kisingefungwa mabao mengi endapo wachezaji wake nane majeruhi wangekuwepo kama vile Christian Benteke, Wilfried Zaha, Ruben Loftus-Cheek na wengine.
Mchezo unaofuata Crystal Palace watakuwa kwenye Uwanja wa nyumbani Oktoba 14 dhidi ya mabingwa watetezi, huo utakuwa mtihani mwingine kwa kocha Hodgson ambaye ana kazi ngumu kuhakikisha timu hiyo inabaki kwenye ligi msimu ujao.