JOSEPH HIZA NA MTANDAO
RIPOTI mpya ya utafiti inaonesha kuwa mamilioni ya wanawake duniani hujifungua kwa njia ya upasuaji badala ya asili, bila ya kuwapo sababu yoyote ya kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapwa hivi karibuni na Jarida la Sayansi la The Lancet, viwango vya dunia vya wanawake kujifungua kwa njia ya upasuaji viliongeza mara mbili kati ya mwaka 2000 na 2015.
Imeelezwa kuwa mara nyingi upasuaji huo ukifanywa bila ya kuwa na umuhimu au manufaa yoyote ya uzazi.
Upasuaji unaweza kuokoa maisha ya wanawake na watoto iwapo kuna matatizo ya uzazi kama kasoro katika kijusi au kijusi kuwa katika hali au mazingira yasiyo ya kawaida.
Hata hivyo, utafiti huo umesema iwapo upasuaji utakuwa chaguo la kila mara kwa wanawake wanaotaka kujifungua bila sababu ya kiafya, huenda ikasababisha athari za muda mrefu na gharama kubwa kwa huduma za afya.
Wataalamu wanatathmini kuwa kati ya asilimia 10 na 15 ya wanawake wanaojifungua kupitia upasuaji kutokana na matatizo ya kiafya.
Kwa kuzingatia takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kutoka mataifa 169, utafiti huo ulibaini tofauti kubwa kati ya maeneo ya kijiografia.
Aidha, asilimia 60 ya mataifa hayo yalitumia vibaya upasuaji na asilimia 25 wakiitumia njia hiyo ya upasuaji kwa kiwango kidogo.
Katika mataifa 15, zaidi ya asilimia 40 ya waliozalishwa walipitia upasuaji, huku Jamhuri ya Dominika ikiongoza kwa asilimia 58.1 ya watoto waliozaliwa kupitia njia ya upasuaji.
Katika mataifa ya Brazil, Misri na Uturuki zaidi ya nusu ya watoto wanazaliwa kupitia upasuaji, na katika maeneo ya Magharibi na Afrika ya Kati upasuaji ulitumika kwa asilimia 4.1 tu.
Utafiti huo wa jopo la madaktari pia umeonesha kuwa upasuaji unaweza kuchangia athari kubwa katika miaka ijayo kukiwamo vizazi vya baadaye.
Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kovu la tumbo, kuharibika kwa mji wa mimba, kondo lisilo la kawaida, ujauzito ulio nje ya mji wa mimba, watoto kuzaliwa wakiwa wamekufa au kabla ya siku zao.
Vilevile imethibitishwa kuwa upasuaji unaweza kuwa na athari kwa homoni, mwili na kinga ya mwili ya mtoto.
Utafiti huo aidha umesema kuwa wanawake wanahamasishwa kujifungua kupitia upasuaji kwa sababu ya matatizo waliyoyapata walipojifungua kwa njia ya kawaida, woga, maumivu au kupungua kwa hamu ya kushiriki mapenzi.
Katika baadhi ya nchi upasuaji umekuwa mtindo na kuchukuliwa kuwa wa kisasa au salama.
Watafiti wanasema kuna haja ya hatua ya haraka kuchukuliwa katika sekta ya afya kupunguza idadi ya wanawake wanaojifungua kupitia upasuaji.
Kadhalika, wamependekeza wanawake wapewe taarifa zaidi na ushauri kuhusu athari za upasuaji, pamoja na kuongezwa kwa huduma ya uzazi na kuhakikisha madaktari wanatoa sababu ya kutosha kabla ya kuamua kumzalisha mtu kupitia upasuaji.
Ripoti hiyo inakuja huku tafiti katika mataifa ya Afrika Mashariki hususani Kenya yakionesha wanawake wengi nchini humo hupendelea kujifungua kwa kisu.
Ni kizazi kipya kinachodai kwamba njia ya kawaida inaambatana na vitu kama vile kuchanika, saa nyingi katika chumba cha uzazi, huduma holela, maumivu ya kisaikolojia na kimwili wakati wa kusukuma na mabadiliko ya ukubwa wa asili wa uke.
Baadhi wanaripoti kesi za matibabu duni zinazofanywa na wafanyakazi wa afya katika baadhi ya hospitali hasa za umma.
Kutokana na matokeo hayo, wanawake hasa wa tabaka la wafanyakazi maeneo ya mijini hutumia bima zao za afya kujifungua kwa njia ghali ya upasuaji.
Lakini kama utafiti mpya unavyoonesha wataalamu nchini humo pia wana wasiwasi unaozidi kuongezeka kwamba upasuaji usio wa lazima unasababisha vifo na athari za muda mrefu kwa kuwaweka wanawake kwa njia iliyolenga matumizi ya dharura tu.
Sababu hizo zinazosababisha wajawazito wengi nchini Kenya kupendelea kujifungua kwa njia ya upasuaji badala ya njia ya kawaida ya kuvumilia maumivu ya uzazi wa watoto wao, zimekuwa zikizua mjadala mkali katika miaka ya karibuni.
Kwa mujibu wa Takwimu za Bodi ya Bima ya Matibabu nchini Kenya (NHIF), katika mwaka wa fedha 2014/2015, kati ya wanawake 61, 420 waliojifungua na kuwasilisha maombi yao ya malipo ya bima kwa hazina hiyo, 20,773 walijifungua kupitia njia ya upasuaji.
Zinaonyesha kuwa asilimia 34 ya wanawake hao waliamua kufanyiwa upasuaji badala ya kujifungua kwa njia ya kawaida.
Katika mwaka wa fedha 2015/16 idadi hiyo iliongezeka kufikia asilimia 42 huku kuelekea mwaka 2017 dalili zilionesha ilifikia hadi asilimia 58. Hii ni kwa mujibu wa takwimu zilizoandaliwa na Mkurugenzi wa NHIF nchini humo, Simeon Kirgotty.
Anapendekeza kuwa Wizara ya Afya itekeleze uchunguzi wake kuhusu suala hilo akisema kuwa labda kuna mtindo wa wanawake wa kuchagua wenyewe kujifungua kupitia upasuaji.
“Kunahitajika utafiti kamili kuhusu suala hilo ili ieleweke kama kwa kweli kujifungua kupitia upasuaji kunaongezeka kufuatia changamoto za kiafya, au ni mtindo sawa na fesheni ambazo wanawake wanakumbatia kwa kasi,” anasema.
Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za uzazi wa wanawake na viongozi wa kidini na wale wa kisiasa wamekuwa wakisaka ukweli wa mambo kuhusu suala hilo.
Katika kongamano lilofanyika hivi majuzi, lililoandaliwa katika Kaunti ya Kiambu likihusisha wanawake, kina mama walifunguka na kuelezea kinaga ubaga ni kwanini hupendelea kujifungua kwa njia ya upasuaji badala ya kawaida.
Wanasema kuwa madaktari wanaowasaidia kujifungua hospitalini huwa hawawashoni kiungo chao cha uzazi baada ya kupasuka wakijifungua, hali ambayo huwaacha wakiwa ‘wamepanuka.’
Wanasema hali hiyo huwavunjia starehe zao za mahaba mbali ya tatizo lingine, ambalo ni kuwafanya watalikiwe na wapenzi wao wa kiume.
Kongamano hilo liliandaliwa katika Mgahawa wa Windor chini ya ufadhili wa Mwinjilisti Rachel Njeri ambaye pia ni mwanamuziki wa nyimbo za injili.
Wageni waalikwa katika kongamano hilo na ambao walionekana kusikiliza suala hilo kwa mshtuko walikuwa ni pamoja na wawakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Nakuru, Mary Mbugua na mwenzake wa Murang’a, Sabina Chege.
Mmoja wa waliohudhuria kongamano hilo, Jane Njogu, alikiri waziwazi kuwa bila madaktari hasa katika hospitali za umma kuwajibika na kutekeleza majukumu yao ya ukunga kwa njia yenye ubinadamu, wanawake wataendelea kujifungua kupitia upasuaji.
“Ni suala la kufedhehesha kuona mwanamke aliyebarikiwa na mtoto akirejea nyumbani katika ndoa yake, lakini badala ya kupokewa kwa furaha kwa kuleta malaika, anaishia kufukuzwa na bwana wake.
“Ni kwa kuwa kiungo chake kimeharibika katika uzazi. Na inatokea mwanamke huyo amekumbwa na changamoto ya kiafya ambapo hupasuliwa na katika harakati ya kuzaa humpa ugonjwa wa fistula,” anasema.
Aidha, Alice Mueni anasema madaktari huwa hawazingatii uchungu ambao humkumba mwanamke wakati wa kuzaa na huwa hawawapi dawa za kupunguza makali ya uchungu huo.
“Kisayansi, imegunduliwa kuwa uchungu huo wa kuzaa huwa ni sawa na ule unaoweza kumkumba mwanamke akivunjwa viungo vya mwili mara 74! Sisi ni binadamu ambao uchungu huo hutuathiri kwa kiasi kikubwa,” anasema.
“Wapo ambao wameishia kurukwa na akili kupitia uchungu huo. Njia ya mkato ni kupendekeza upasuaji ili ukichomwa sindano za kudhibiti maumivu, unajifungua bila shinikizo,” anashauri.
Anasema hali nyingine ambayo huchangia kupendelea upasuaji wakati wa kujifungua ni kuwa, kiungo cha uzazi hubakia salama na “kinachoweza kuendelea kutumika na mpenzi wako.”
Alisema: “Ikiwa mumeo atakuwa na haraka ya kuendelea kuburudika kimahaba, basi hatakuwa na muda mrefu wa kusubiri kwa kuwa kiungo hicho hakijaathirika. Kidonda kinachoachwa na upasuaji hupona haraka na bwana wako hatapotea bomani akisaka kwa kujiburudisha huku ukiuguza kiungo chako cha mahaba.”
Kwa mujibu wa WHO, upasuaji unapaswa kufanyika iwapo tu mjamzito au mtoto aliye tumboni ana tatizo la kiafya, vinginevyo, unaweza kuwa na athari pindi unapofanyika na hata baadaye.
Hatari za kujifungua kwa njia ya upasuaji ni pamoja na mtoto kuwa na matatizo ya kupumua, kuumizwa, ingawa ni mara chache kutokea.
Kwa mama hukumbwa na maambukizi ya tumbo la uzazi (endometritis), kupoteza damu nyingi, damu kuganda kwenye mishipa ya kiuno au miguu, kidonda kupata maambukizi, kuchelewa kupona au kufumuka.
Wakati mwingine kibofu cha mkojo kinaweza kuumizwa wakati upasuaji unafanyika.
Mwisho.