RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MKURUGENZI wa Haki Elimu, Dk.John Kalage amesema mambo manne yanamkwamisha mtoto wa kike kufikia ndoto zao,ikiwamo ndoa za utotoni.
Alitoa kauli hiyo jijini Dodoma juzi, wakati wa majadiliano kuhusu changamoto zinazomkwamisha msichana kufikia ndoto zake na nini kifanyike,pia Azaki zimefanya na zinapaswa kufanya nini kumkomboa msichana.
Majadiliano hayo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya Azaki inayoendelea jijini hapa.
Alisema zaidi ya watoto milioni 15 huolewa kila mwaka kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo hali ambayo imekuwa ikisababisha kutofikia ndoto zao.
Alisema sababu nyingine, ni mimba za utotoni ambapo alidai zaidi ya wasichana milioni moja huolewa kabla ya kufikisha miaka 15.
“Changamoto nyingine, ni mazingira ya shule kutokuwa rafiki, unakuta mtoto wa kike yupo katika hedhi anashindwa kuendelea na masomo,wakati mwingine wengine wanatembea umbali mrefu kufuata elimu, huku sehemu zingine miundombinu sio rafiki,”alisema.
Alisema utumikishwaji wa watoto hasa wadada wa kazi, jambo ambalo limekuwa likiwafanya washindwe kufikia ndoto zao.
Alisema pia wazazi kutotoa haki sawa kwa watoto ambapo baadhi ya wazazi na walezi hujikuta wakiwapendelea watoto wa kike katika suala la elimu.
“Tumeona uandikishwaji wa watoto upo juu katika shule za msingi,kadri unavyopanda katika elimu ya juu unaona kabisa idadi inapungua, zinahitajika jitihada za dhati kuhakikisha mtoto wa kike nasaidiwa kupata elimu,”alisema.
Alisema sheria ya mtoto ya mwaka 2009,sheria ya elimu ya mwaka 1974 na sera ya mwaka 2004, zinazungumzia kuhusiana na mtoto wa kike kulindwa.
‘Mila na desturi nazo zimekuwa ni kikwazo kufanikisha ndoto za mtoto wa kike ,”alisema.