GAZETI dada la MTANZANIA Jumamosi la jana, liliripoti juu ya simulizi ya kuhuzunisha ya mwanamke aliyetambulika kwa jina la Amina Mbunda, mkazi wa Kijiji cha Mgudeni, mkoani Morogoro, ambaye alilazimika kujifungulia kituo cha polisi baada ya kukosa msaada.
Inaelezwa hatua ya Amina kujifungulia polisi ilitokana na askari wa kituo cha Mang’ula kumweka mahabusu baada ya kushindwa kumpata mumewe wanayemtuhumu kwa kununua kitanda cha wizi.
Inaelezwa askari hao ambao walikuwa wameongozana na mgambo wa kijiji hicho, walimchukua kwa nguvu Amina ambaye alikuwa tayari ameanza kusikia dalili za kuumwa uchungu.
Tukio hili limezua gumzo na hata baadhi kutaka kujua kama sheria inaruhusu kumkamata mtu mwingine baada ya mtuhumiwa kukosekana.
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na vyombo vya habari, wamesema jambo hilo halipo kisheria.
Matukio ya namna hiyo au yanayofanana na hayo si mara ya kwanza kuripotiwa na vyombo vya habari.
Ipo orodha ndefu ya watu kusingiziwa kesi, kukutwa na madhila makubwa mikononi mwa polisi, mfano ni tukio la hivi karibuni lililotokea mkoani Mwanza ambako mama mmoja aliyekuwa akituhumiwa kumwibia simu jirani yake, alimpoteza mtoto mdogo baada ya kuugua na kuzidiwa akiwa mahabusu.
Tukio kubwa na ambalo bado halijatoka katika vichwa vya wengi, ni lile la Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, kuuawa wakati Jeshi la Polisi likizuia maandamano ya Chadema.
Ingawa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, alisema jalada la kesi hiyo limefungwa kwa hoja kwamba katika maandamano hayo kulikuwa na watu zaidi ya 200, hivyo ni vigumu kubaini aliyehusika kumpiga risasi Akwilina, lakini pia mwili wake haukutolewa risasi yoyote.
Kauli hiyo bado imeacha sintofahamu na kuzua maswali mengi juu ya aliyehusika na kifo cha mwanafunzi huyo.
Pamoja na hayo yote, bado tunakumbuka kauli aliyopata kuitoa Rais Dk. John Magufuli, wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alipokutana na makamanda mikoa yote, viongozi na wakuu wote wa jeshi hilo mara baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Katika kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Rais Dk. John Magufuli, alimtaka IGP huyo mpya pamoja na safu yake ndani ya Jeshi hilo kujipanga vizuri kwa maana ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji.
Tuliandika huko nyuma kwamba kauli ambayo ilitugusa na bado imeendelea kutugusa, ni ile aliyosema kwamba anataka kuona Jeshi la Polisi linakuwa Jeshi la Polisi, akitoa wito kwa Sirro na wenzake kuhakikisha wanarudisha hadhi na heshima ya chombo hicho kwa kukomesha uhalifu.
Tunaona kauli hii inaendelea kutugusa hadi sasa kwa sababu msingi hasa wa kuanzisha Jeshi la Polisi ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.
Leo hii tunapoona baadhi ya askari wa jeshi hilo kwa kujua ama kutojua wanakwenda tofauti na misingi hiyo, inatupa shida na hata kujiuliza kama walinda amani hawa kama kweli mafunzo wanayoyapata wanayafanyia kazi ama la!
Kauli aliyopata kuitoa Rais Magufuli akitamani kuona Jeshi la Polisi linafanya kazi yake sawasawa ya kulinda raia na mali zao na pengine kuliko ilivyo, inapaswa kuwa kama sala ya kila siku kwa askari wetu.