NA ATHUMANI MOHAMED
NILIANZA mada hii wiki iliyopita, ambayo kwa hakika ni muhimu sana katika maisha maana ni ukweli usiopingika kuwa sehemu kubwa ya muda wetu, tunatumia kazini.
Hii inamaana kuwa, ikiwa tutashindwa kujua mambo muhimu zaidi ya kuzingatia mahali pa kazi, basi furaha ya maisha yetu kwa jumla itakuwa shakani.
Katika utangulizi wa makala haya kwenye sehemu ya kwanza wiki iliyopita nilieleza kuhusu umuhimu wa kuheshimu bila kubagua, ubunifu kazini na ushirikiano.
Hayo yalikuwa mambo matatu kati ya saba ya kuzingatia. Leo tunamalizia mambo manne yaliyosalia ambayo nina hakika kwamba yatakuongoza kwenye ubora sehemu ya kazi.
JIFUNZE KWA WENGINE
Kuwa msikilizaji zaidi kuliko mwongeaji. Mara nyingi msikilizaji huvuna zaidi mawazo ya wenzake kuliko yule anayependa kusikilizwa zaidi yeye.
Wapenda kusikilizwa, wakikutana na mtu mwenye kupingana kwa hoja mwisho wake huwa ugomvi usio na lazima. Pendelea zaidi kujifunza na hata inapotokea unataka kueleza msimamo wako, basi uwe na hoja zenye nguvu na mashiko.
Tumia lugha nzuri katika kuwasilisha unachokiamini huku ukitumia mifano halisi badala ya mabavu. Hii haijalishi majukumu yako, nafasi yako kazini na juhudi yako.
Ukionyesha ujuaji kupitiliza ni dhahiri kuwa utajiwekea wigo wa marafiki, wengi watakudharau na kukutenga kutokana na tabia yako hiyo.
HESHIMU MAAMUZI YA WENGI
Inawezekana kumekuwa na mjadala fulani juu ya maamuzi ya jambo fulani kiofisi. Unayo nafasi ya kutoa mawazo yako, lakini using’ang’anie yawe sheria hata kama wenzako wengi wanakupinga kwa hoja.
Kama wengi wanakataa, na wewe umebaki peke yako na msimamo wako, ni wazi kuwa utatakiwa kufuata yale yaliyoafikiwa na wengi. Acha uking’ang’anizi, hautakusaidia.
Zaidi utakuweka mbali na wenzako wanaopenda demokrasia. Waswahili wanasema, sauti ya wengi, ni sauti ya Mungu. Toa nafasi kwa wenzako. Acha ubinafsi na kuamini zaidi mawazo yako.
ACHA LAWAMA
Unapokuwa mahali pa kazi, kuna wakati hutokea ukaadhibiwa kutokana na makosa ya hapa na pale makazini. Ni vizuri kuwa muelewa na kukubaliana na maamuzi ya viongozi wako.
Hata kama katika tafakuri yako umegundua kuwa umeadhibiwa kwa uonevu au ulisingiziwa mambo mabaya, usimlaumu mtu yeyote wa kazini kwenu. Jipe muda, tulia.
Acha kuongea sana na watu kuhusiana na kupewa kwako adhabu. Hata ikitokea mtu anakuchimba akitaka kujua kilichotokea usimpe nafasi hiyo kabisa.
Hao ni wachonganishi ambao wanaweza kuchukua maneno kwako na kuyarudisha kwa bosi wako, jambo ambalo linaweza kukuharibia kibarua chako.
USIMSEME MWAJIRI WAKO
Mwingine akiadhibiwa anakimbilia kumsema vibaya mwajiri wake, si jambo zuri. Kulalamika kuwa umeonewa au kumsema bosi wako kuwa amekufanyia mtimanyongo kukuadhibu hakutakusaidia kitu, zaidi unajiharibia.
Wapo wanaofikia hatua hata ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii maneno ya kuwaponda ama waziwazi au kwa mafumbo mabosi wao.
Hilo si jambo lenye maana sehemu za kazi, bali unaharibu mustakabali wako wa kazi siku zijazo. Kumbuka mitandao ya kijamii inatembelewa na watu wengi.
Huenda bosi wako ajaye naye ni miongoni mwa watakaosoma namna unavyomshambulia bosi wako. Je, ni nani atakayekupa nafasi kwenye ofisi yake wakati ameshaona namna unavyomshambulia bosi wako wa sasa? Kuwa makini sana na hilo.
Mada yetu imeishi hapa. Tukutane wiki ijayo katika mada nyingine.