32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO 10 YAVURUGA DAWA ZA KULEVYA

Na MWANDISHI WETU,

MAMBO kumi yamedhihirika kubadili upepo wa vita dhidi ya dawa za kulevya iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika kipindi cha ndani ya mwezi mmoja.

Februari 2, Makonda alitaja kwa mara ya kwanza majina ya baadhi ya wasanii, akiwamo Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na askari polisi aliodai wanahusika na dawa za kulevya, na siku sita baadaye, akataja majina mengine 65, yakiwamo ya wanasiasa na watu wengine maarufu, akiwataka wafike Kituo  Kikuu cha Polisi wakajadiliane juu ya tuhuma hizo.

Wakati leo ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu sakata hilo liibuke na kuibua hoja kinzani katika jamii, taasisi mbalimbali zikiwamo za kiserikali na ndani ya Bunge, suala la elimu ya Makonda ni miongoni mwa mambo ambayo yameonekana kuteka kwa kiasi kikubwa mijadala ya sasa na hata kujenga hisia za au kuchepusha ama kubadili upepo wa vita hiyo.

Kumekuwa na maneno mengi kuhusu elimu ya mkuu huyo wa mkoa na majina yake halisi.

Mjadala huo ambao ulipata kuibuka mwaka 2012 wakati Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wakiwa katika uchaguzi wao,  kuibuka kwake sasa chimbuko lake ni mitandao ya kijamii kabla Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuupa nguvu wiki iliyopita kwa kuamua kuzungumza jambo hilo hadharani.

Askofu Gwajima ambaye alizungumza suala hilo kama njia ya kulipiza kisasi baada ya Makonda kumtaja katika sakata la dawa za kulevya, alikwenda mbali na kusema anao ushahidi juu ya kile alichodai kuwa kiongozi huyo ana utata kuanzia elimu hadi majina yake.

Gwajima alidai kuwa majina halisi ya kiongozi huyo ni Daudi Albert Bashite na kwamba jina la Paul Makonda lilipatikana baada ya kuamua kutumia cheti cha mtu mwingine baada ya kufeli mtihani wa kidato cha nne.

Si Makonda wala mamlaka yake ambayo imepata kulizungumza kwa undani suala hilo, zaidi yeye mwenyewe kupuuza taarifa hizo kila anapoulizwa na vyombo vya habari.

Kabla ya hapo, Makonda huyo huyo siku chache baada ya kutangaza majina ya watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuingia katika mgogoro na baadhi ya wabunge ambao walikuwa wakipinga utaratibu alioutumia wa kuwataja hadharani watuhumiwa hao, iliibuka hoja ya kutaka naye achunguzwe kwa madai ya kupata ukwasi wa kutisha ndani ya kipindi kifupi.

Hatua hiyo ambayo ilionekana kubadili upepo kwa kiasi chake kutokana na kuchukua mijadala mikubwa katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ilichagizwa na hoja za wabunge, Joseph Selasini (Chadema) na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ (CCM).

Selasini ambaye ni mbunge wa Rombo, alikwenda mbali na kutaja mali zinazodaiwa  kumilikiwa na mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Akichangia taarifa za kamati za Bunge za Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Selasin alisema Makonda amenunua jengo  (apartment) lenye thamani ya shilingi milioni 600.

“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa shilingi milioni 600, Makonda amempa mke wake gari aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Dola 250 za Marekani (shilingi milioni 550) kama zawadi ya birthday,” alisema Selasini.

Siku moja kabla ya Selasini kusema hayo, Msukuma ambaye ni mbunge wa Geita Vijijini, naye aliibuka na tuhuma nyingine nzito dhidi ya Makonda na kutaka vyombo husika vichunguze.

  “Anatumia Lexus ya petroli ya Sh milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa Serikali.

“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa… ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na hawa mawaziri tulionao humu, kwanini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria kwanini mmepigwa ganzi?” alisema.  

Msukuma pia alihoji Makonda alikopata fedha za kwenda Paris na Marekani na kukaa siku 21, hasa ikizingatiwa kuwa tiketi moja ni Dola za Marekani 14,000  huku yeye na mkewe jumla ikiwa ni dola 28,000.

Mbali na hayo, uamuzi wa mwanzo kabisa alioufanya Rais Dk. John Magufuli wa kumteua Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga ni kielelezo kingine ambacho kilibadili upepo wa vita aliyoanza nayo Makonda.

Tofauti na Makonda ambaye mapambano yake aliyaendesha kwa kutaja hadharani watuhumiwa, chini ya Kamishna Siyanga, majina ya watuhumiwa hayatangazwi hadharani badala yake wanachunguzwa na kukamatwa kimya kimya.

Itakumbukwa kuwa kuteuliwa kwa Siyanga na wasaidizi wake wawili kulitokana na hoja zilizoibuliwa na baadhi ya wabunge ambao walitaka jambo hilo litekelezwe kwa kufuata misingi ya sheria hususani ile ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2015 kwa kile walichodai kuwa alichokuwa akikifanya Makonda kilikuwa hakina misingi ya kisheria.

Februari 14, mwaka huu baada ya Kamishna Siyanga kukabidhiwa majina 97 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya na Makonda, aliahidi kutotangaza watuhumiwa hadharani na badala yake watayafanyia uchunguzi na pale watakapobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Si hilo tu, hatua ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwapiga marufuku wakuu wa mikoa kutotangaza majina ya watuhumiwa pasipo kufuata taratibu za kisheria, nayo ilionekana kuchepusha upepo.  

Itakumbukwa uamuzi huo wa Waziri Mkuu, ambao alioutoa wakati akizindua Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, ulikuja wakati ambao vita hiyo ilikuwa imepamba moto na kuonekana kuchukua sura ya kitaifa.

Ni wakati huo ndio ambao Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa msimamo wa kugoma kufika kuhojiwa na vyombo vya dola akitaka taratibu za kisheria zifuatwe.

Mbowe ambaye alitajwa katika orodha ya watuhumiwa 65 wa sakata hilo, uamuzi wake huo na ule wa kukimbilia mahakamani kufungua kesi ya kikatiba dhidi ya Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa kanda hiyo, Camillius Wambura, unatajwa kama miongoni mwa mambo ambayo yamechangia kufifisha vita hiyo.

Tukio hilo la Mbowe la kufungua kesi ambalo lilikwenda sambamba na uamuzi wa Wema kutangaza kuhama CCM na kuhamia Chadema lilionekana kujenga hisia ya kuchukua zaidi mwelekeo mwingine mpya wa kisiasa.

Si hilo tu, tukio jingine lililoonekana kubadili sura ya vita hiyo ni hatua ya Jeshi la Polisi kuwaona hawana hatia Askofu Gwajima, aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Iddi Azzan na wengine licha ya Makonda kupata kueleza kuwa anao ushahidi wa miaka kumi baada ya kuwafuatilia watuhumiwa hao wa dawa za kulevya.

Tukio jingine lililobeba sura hiyo ni kukamatwa na kuwekwa ndani kwa baadhi ya watuhumiwa ambao walitajwa katika orodha ya wafanyabiashara, lakini baadaye wakafikishwa mahakamani na kushtakiwa kama watumiaji, huku wengine wakiwekwa chini ya uangalizi wa polisi pasipo kushtakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles