Na Aziza Masoud,
KATIKA jamii kwa sasa kumekuwa na wimbi la watoto wanaolelewa na mzazi mmoja kutokana na sababu mbalimbali.
Katika nyakati hizi, idadi ya watoto ambao wanakuwa katika familia zilizo katika uangalizi wa chini ya mzazi mmoja, inadaiwa kuongezeka, hususan mama.
Famili hizo zimeongezeka sana hata kufikia idadi sawa au zaidi ya familia zenye baba na mama wanaoishi pamoja katika jamii nyingi.
Kuna sababu nyingi zinazochangia hali hiyo, zikiwamo kifo, utelekezwaji wa familia, kuhamishwa kikazi, masomo, hususani elimu ya juu n.k na kusababisha mtoto kulelewa na mzazi mmoja.
Malezi ya mzazi mmoja pamoja na kuwa yana sababu, lakini yanakuwa na changamoto nyingi, ikiwamo ufinyu wa kipato, kukosa ushirikiano kutoka kwa mzazi wa kufikia, upweke unaopelekea msongo wa mawazo n.k.
Malezi haya husababisha watoto kuwa wapweke na kuhisi kwamba mzazi anayekuwa naye kwa wakati huo ndiye anayemhusu zaidi.
Wapo wazazi ambao wanaishi mbali na watoto wao mpaka inafikia hatua ya mtoto kutomtambua kama ni baba ama mama yake kupitia hisia na badala yake mpaka atakapoambiwa na mtu aliyekuwa naye karibu.
Hali hii ni mbaya sana, maana humfanya mtoto kutengeneza chuki na mzazi fulani, huku mwingine akiishi kama hana mzazi.
Wazazi lazima watambue kuwa karibu na mtoto kunasaidia kutengeneza muunganiko ambao unachangiwa na hisa baina ya mtoto na mzazi zinazotokana na ukaribu wao.
Ili kuondoa hali hii, ni vema ukajenga mazingira ya ulezi shirikishi, unalea mtoto wako huku ukimshirikisha mzazi mwenzako, hata kama hana kitu.
Ni vigumu kulea mtoto bila msaada hata kama sio wa kifedha, ushauri nao hujenga watoto.
Mzazi husika unapaswa kusema unataraji nini katika malezi ambayo mnachangia na mwenzako, ili isaidie kumuweka mtoto katika njia sahihi.
Siku zote watoto huwa na furaha na amani ikiwa watakuwa na mahusiano mazuri na ya karibu baina yao na wazazi wao.
Mzazi hata kama atakuwa anaishi mbali anapaswa ahakikishe anapata muda kwa ajili ya kumuona mtoto na kuongea naye hata mara moja kwa wiki.
Pia unaweza ukatumia muda wako mdogo kumtoa out kwa ajili ya kuangalia mazingira sehemu mbalimbali, kusoma, kutembea, kuimba n.k.