27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Malawi: Hakuna mjadala Ziwa Nyasa

Rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika
Rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Malawi, Profesa Peter Mutharika, kwa mara nyingine amesisitiza kuwa Ziwa Nyasa linamilikiwa na nchi yake.

Kutokana na hali hiyo, amesema katu uongozi wake hautarajii kukaa katika meza ya majadiliano na nchi jirani ya Tanzania kuzungumzia umiliki huo.

Mutharika alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Lilongwe kuhusu ziara yake ya hivi karibuni jijini Washington DC, Marekani ambako alikuwa akishiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika na Marekani.

“Ziwa hilo limekuwa letu kwa miaka 104, sheria iko wazi, nadhani kuna nafasi ndogo ya majadiliano kuhusu suala hili,” alisema.

Hata hivyo, Mutharika aliondoa uwezekano wa kuingia vitani na Tanzania, akisema ana dhamira ya dhati kutatua mgogoro huo kwa amani pamoja na rais mwenzake wa Tanzania.

Alieleza namna walivyokutana na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, kwamba alipata nafasi ya kumkaribisha kutembelea Malawi na kuvua samaki pamoja naye ziwani.

Mgogoro kuhusu ziwa hilo ambalo linajulikana kama Ziwa Malawi nchini Malawi na Ziwa Nyasa nchini Tanzania, ni wa muda mrefu, lakini uliongezeka baada ya Rais wa zamani wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika, kuingia mkataba na kampuni ya Uingereza kutafiti uwezekano wa kuwapo akiba ya mafuta ziwani humo.

Kwa sasa mgogoro huo unasuluhishwa na kamati ya viongozi wa zamani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakiongozwa na Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chisano.

Kauli hiyo ya Mutharika ni ya kwanza tangu aingie madarakani Mei 31, mwaka huu ingawa wakati wa kampeni za uchaguzi aliwahi kukaririwa akisema kuwa hatarajii kupoteza muda kujadili na Tanzania kitu ambacho kinajulikana wazi mmiliki wake, akimaanisha ziwa hilo lote ni mali ya Malawi.

Ikitumia makubaliano ya kikoloni ya mwaka 1890, Malawi inadai kumiliki ziwa lote, ambalo inaaminika lina akiba ya gesi na mafuta, huku Tanzania ikisisitiza mpaka wake unaangukia katikati ya ziwa hilo.

Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda, aliyeshindwa na Mutharika katika uchaguzi wa Mei, mara kwa mara alikuwa akitishia kulipeleka suala hilo katika Mahakama ya Sheria ya Kimataifa.

Julai 20, mwaka huu, Rais Kikwete, alisema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo.

Alisema Tanzania haioni mantiki ama busara kuingia vitani na nchi jirani kwa sababu yoyote ile.

Kauli hiyo aliitoa alipokuwa anahutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa mjini Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa.

“Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita, laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita.

“Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka. Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita. Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya majadiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee, bali kwa mipaka yote ya Tanzania,” alisema.

Awali mgogoro huo ulishika kasi hali iliyolifanya Bunge kuingilia kati kupitia Kamati ya Mambo ya Nje chini ya Mwenyekiti wake Edward Lowassa, ambapo liliitaka Serikali kutumia diplomasia kuumaliza.

Mgogoro huo hivi sasa unashughulikiwa na jopo la marais wastaafu;

Joachim Chissano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wanaosaidiwa na jopo la kimataifa la mabingwa wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles