27.7 C
Dar es Salaam
Monday, December 16, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda: Wasiooga marufuku kukanyaga Dar

NORA DAMIAN Na BRIGHITER MASAKI – DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amepiga marufuku watu wasiooga na kuwa nadhifu kuingia katikati ya jiji hilo wakati wa mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) mwezi ujao.

Tayari vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 wamesambazwa maeneo mbalimbali ya jiji hilo kusimamia usafi wa mazingira.

Akizungumza jana wakati wa kuzindua kampeni ya usafi wa mazingira kama sehemu ya maandalizi ya mkutano huo, Makonda alisema wamejipanga vyema, hasa katika suala zima la usafi kuepuka kumtia aibu Rais Dk. John Magufuli mbele ya marais wenzake.

“Wakati wa mkutano huu hatutarajii kuona watu wachafu mtaani. Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga, hujanyoosha nguo ni marufuku, mpumzike tu majumbani kwenu.

“Kwa kipindi hiki tuvumiliane, kama hufui nguo, huogi, pumzika kidogo kuja mjini usitutie aibu, na siyo kwamba tunataka usafi tu wa mazingira hapana, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa,” alisema Makonda.

Pia aliagiza kuanzia sasa wenye magari binafsi watakaotupa taka ovyo wasitozwe faini badala yake wapewe eneo la kufanya usafi kwani baadhi yao wamekuwa na jeuri ya fedha na kwamba kwao faini si adhabu.

Ule utaratibu wetu wa Lugalo tunauanza leo (jana) kwenye barabara zote ndani ya mkoa, haiwezekani mtu uwe na nidhamu kwenye kile kipande cha mita 200 – 300 halafu hiyo nidhamu ukifika kwingine inapotea.

“Kwa hiyo kwa mtu mwenye gari anayetupa taka ovyo barabarani, kuanzia leo mshusheni, akikataa kusimama chukueni namba ya gari toeni taarifa, tutamkamata aje kufanya usafi kwa kupiga deki,” alisema Makonda.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usafi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri, alisema shughuli za usafi zimeanza jana kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na maeneo mengine ya jiji, na kwamba wakandarasi na halmashauri za manispaa zimetoa vifaa mbalimbali yakiwemo magari kufanikisha shughuli hiyo.

ILIVYOKUWA ZIARA YA OBAMA

Kumbukumbu zinaonesha licha ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na mikakati mbalimbali ya usafi wa mazingira, lakini limekuwa likiongeza jitihada zaidi pindi kunapokuwa na ugeni mkubwa kama ilivyokuwa kwa ziara ya Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama mwaka 2013.

Obama alifanya ziara ya siku mbili nchini na kabla ya ujio wake kulikuwa na hekaheka kubwa ya kuandaa mazingira kwa ugeni huo.

Sehemu nyingi za barabara zilitengenezwa usiku na mchana, mitaro iliyokuwa imejaa majitaka ilizibuliwa, nyasi zilifyekwa, kuziba mashimo sambamba na kuondoa taka zilizokuwa zimezagaa maeneo mbalimbali ya jiji.

Barabara alizopita Obama zilifanyiwa matengenezo madogo madogo, hususani zile zilizokuwa na mashimo, huku nyingine zikiwekewa taa za barabarani na baadhi ya wamiliki wa majengo katika sehemu alizopita walilazimika kuyapaka rangi.

WIKI YA VIWANDA

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, ameagiza kila aliyeomba kushiriki maonyesho ya Wiki ya Viwanda kwa wanachama wa SADC apewe fursa.

Maonyesho hayo yanatarajiwa kuanza Agosti 5 hadi 9 viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Balozi Kijazi ambaye aliongozana na Katibu Mkuu Kiongozi – Zanzibar, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na kamati ya maandalizi, alikuwa akizungumza jana baada ya kukagua kumbi mbalimbali zitakazotumika wakati wa mkutano huo.

“Idadi ya walioomba imekuwa kubwa kuliko tulivyotarajia, na kwa kila aliyeomba tumpe fursa kwa sababu nia yetu pia ni kutangaza bidhaa zetu, kwa kufanya hivyo wageni watakaokuja watajua kuna ‘product’ gani watazipata hapa nchini kutoka kwa wajasiriamali wetu.

“Tumeshateua maeneo ambayo maonyesho yatafanyika kuzunguka ukumbi huu (JNICC), Karimjee na Gymkhana pia kutakuwa na mabanda ya maonyesho,” alisema Balozi Kijazi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, hadi sasa zaidi ya wafanyabiashara 800 wamejiandikisha kushiriki maonyesho hayo.

Aliwataka Watanzania kuonesha ukarimu kwa wageni watakapofika nchini ili wafanye shughuli kwa amani na kuondoka na sifa njema.

“Wasiondoke na sifa ya kufanyiwa vurugu ama kuporwa vitu vyao, matukio ambayo yanaharibu sifa ya nchi yetu. Wananchi wanatakiwa waelewe wasifikiri kwamba ni tukio la wakati mmoja.

 “Tuna mwaka mzima wa kuwa mwenyeji na kwa mwaka mzima nchi zote za SADC watakuwa wanakutana hapa (Tanzania), kwa hiyo kiuchumi ni fursa kubwa,” alisema.

Pia alivitaka vyombo vya habari viripoti mkutano huo kwa mtazamo chanya wa kujenga na kuipa sifa nchi badala ya kuwa wakosoaji.

“Tusiwe wa kwanza kukosoa au kuonesha kwamba tumeshindwa, sisemi mambo yatakwenda vibaya, lakini kuna watu wengine kawaida yao ni kukosoa tu. Yale mazuri hayasemwi, yanatafutwa yale madogo madogo, tuache huo utamaduni hautusaidii, unatuharibia nchi yetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles