28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda aungwe mkono kusaidia watoto

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekuwa na kampeni ya kusaidia watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo.

Kupitia kampeni hii kwa kushirikiana na wadau wengi, Makonda ameweza kusaidia watoto 45 kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya  Jakaya Kikwete. 

Huu ni msaada mkubwa ambao unaonyesha namna watoto wanavyotakiwa kusaidiwa.

Jana Makonda alikabidhi Sh milioni 34.5 kwa taasisi hiyo kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaotoka familia masikini. 

Fedha hizi zilitolewa kwa ushirikiano na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul maarufu Diamond na wasanii wenzake ili kuunga mkono juhudi za Makonda.

Sisi wa MTANZANIA tunasema juhudi hizi ni nzuri.

Pamoja na mambo yote, Makonda anasema ushirikiano anaoupata utasaidia kuhakikisha watoto wanapata huduma na kuendelea na maisha yao kama wengine. 

Tunakumbuka alipoanza kampeni hii, alisisitiza kuwa angeweza kusaidia watoto 60 ambao wanakabiliwa na matatizo ya moyo. Jambo hili si dogo linapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania anayeguswa na afya za watoto hawa ambao wanateseka na hawawezi kuendelea na mambo mengine yakiwamo masomo.

Moyo unaonyeshwa na Makonda, wasanii na Watanzania wengine, hakika unatoa taswira katika jamii kuwa wapo watu wenye uhitaji mkubwa, lakini wameshindwa kutokana na kipato duni.

Tunasema hivi kwa sababu maeneo mengi si ya mijini tu, bali hata vijijini kuna watoto wengi wenye mahitaji haya, ambao wakati mwingine wanapoteza maisha kwa wazazi kutokuwa na uwezo.

Tunasema hili litawezekana tu kama viongozi wengine wa maeneo mbalimbali, wataungana na kusaidia watoto wenye mahitaji pindi wanapotambua au kupata taarifa.

Kwa kufanya hivi, kutaokoa watoto hawa ambao kesho na keshokutwa ndio wataalamu tegemewa katika taifa letu.

Tunawapongeza wasanini wengine Irene Uwoya, Juma Jux, Mboso, RayVann na Queen Darleen ambao nao wamechangia gharama za kusaidia watoto hawa. 

Huu ni mfano mzuri ambao unaonyeshwa na wasanii hawa kuhakikisha upasuaji huu unafanikiwa.

Pamoja na kumpongeza Makonda na wenzake, pia tunaipongeza Taasisi ya JKCI chini ya Profesa Mohamed Janabi kwamba imeonyesha kazi kubwa inayoifanya na kuokoa gharama za mamilioni ya fedha kama watoto hawa wangepelekwa nje ya nchi.

Kama alivyosema Profesa Janabi kwamba katika kila watoto 100 wanaozaliwa, mmoja ana ugonjwa wa moyo ni jambo la kushtua ambalo linaonyesha namna gani tatizo bado ni kubwa.

Sisi MTANZANIA, tunapenda kuchukua fursa hii kumpongeza Makonda na timu yake katika suala hili na kuwaomba watu wengine wenye uwezo wajitokeze kuwasaidia watoto hawa.

Tunasema hivi kwa sababu, hata vitabu vitakatifu vinasema kutoa ni moyo, tunaamini wapo Watanzania wengi ambao wanaguswa na mateso haya ambayo watoto wanayapitia kila siku katika maisha yao.

Tunawahimiza wasani zaidi waendelee kujitokeza bila kuchoka ili kuionyesha jamii upendo wao hata wakati wa matatizo na si kusubiri wakati wa furaha.

Tunamalizia kwa kushauri Makonda na washirika wake waungwe mkono katika hili kwa maana tunatambua kuna familia ambazo haziwezi kuhimili gharama ya Sh milioni 8.4 kwa matibabu ya mtoto mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles