Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema kuwepo kwa viumbe wageni nchini kumeathiri sekta za kiuchumi zikiwamo utalii, usafirishaji, kilimo, mifugo na nishati itokanayo na maji na uvuvi.
Kutokana na hali hiyo, ametaka hatua za makusudi zichukuliwe kukabiliana na janga hilo ili kuokoa mazingira na uchumi wa nchi.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 28, katika uzinduzi wa kikosi kazi cha kutatua changamoto za viumbe wavamizi ambacho kazi yao kubwa ni kuchambua kwa kina tafiti na miradi mbalimbali ili kuleta suluhisho la tatizo hilo.
Kikosi hicho chenye jumla ya watu 16 kinachojumuisha wataalam mbalimbali kinaongozwa na mwenyekiti wao ambae ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Ezekiel Mwakalekwa.
“Tumekusanyika hapa kwa sababu moja ambayo ni kuunganisha nguvu si tu kuokoa mazingira yetu, bali kuokoa uchumi wa nchi yetu, janga hili si la sekta moja kama tulifanya makosa huko nyuma kushughulikia jambo hili tuache, sekta na taasisi zote zifanye kazi kwa pamoja kwa kupeana taarifa na mikakati ya kukabiliana na changamoto hii viumbe wavamizi sasa ni janga la kitaifa,” amesema.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira na Muungano January Makamba, amesema kuundwa kwa kikosi hicho kulitokana na mapendekezo ya mkutano uliofanyika jijini Arusha Septemba 4, mwaka huu na lilikuwa ni agizo la Makamu wa Rais na waligundua moja ya malalamiko ya wafugaji, wakulima na wavuvi ni kuwepo kwa baadhi ya mimea vamizi katika maeneo yao.
“Tishio kubwa la hifadhi ya Ngorongoro ni kuwepo kwa mimea ambayo wanyama hawawezi kula na sio tu hapo lakini hata katika hifadhi za Serengeti na Saadan hali ipo hivo pia,” amesema Makamba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Profesa Dos Santos Silayo, amesema uwepo wa viumbe hao unatokea kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo shughuli za kibinadamu, maendeleo ya mfumo wa usafiri duniani akitolea mfano meli, mizunguko ya wanyama kutoka eneo moja na jingine na mabadiliko ya tabia nchi pia huchangia kuleta viumbe wavamizi.