ISIJI DOMINIC
JUMANNE ya wiki iliyopita, Rais Uhuru Kenyatta, alimteua Waziri wa Usalama wa Ndani, Dk. Fred Matiang’i, kusimamia kamati ya maendeleo, utekelezaji na mawasiliano katika Baraza la Mawaziri ikimaanisha mawaziri wengine wote watakuwa chini yake.
Kwenye agizo kuu la kwanza la Rais mwaka huu (executive order number one 2019), Dk. Matiang’i atakuwa akiripoti kwa Rais Uhuru moja kwa moja kuhusu utendaji kazi wa kila waziri serikalini jambo lililowaacha maswali watu wengi hususani wanasiasa wakitaka kujua nafasi ya Naibu Rais, William Ruto.
Katiba ya Kenya Ibara 147 inaainisha majukumu ya Naibu Rais ikisisitiza ndiye msaidizi mkuu wa Rais na atasimamia utekelezaji wa kazi za Rais. Aidha Naibu Rais atafanya kazi zilizoelekezwa kwa mujibu wa Katiba na kazi nyingine atakazopangiwa na Rais.
Katika agizo hilo kuu alilotangaza Rais Uhuru, kamati hiyo chini ya Matiang’i itajulikana kama Kamati ya Taifa ya Utekelezaji wa Maendeleo na Mawasiliano ya Baraza la Mawaziri ambayo pia itashirikisha Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki na Katibu wa Baraza la Mawaziri, Joseph Kinyua.
Matiang’i ambaye amekuwa miongoni mwa mawaziri waliodumu kwa muda mrefu ndani ya Serikali ya Rais Uhuru, anasifika kwa misimamo thabiti hadi kupachikwa jina ‘Mr Fix It’. Ni mchapa kazi asiyependa kutaka maamuzi yake kuonekana kama ya kisiasa.
Katika kila wizara ambayo ameteuliwa, Wakenya wamekuwa wakishuhudia mabadiliko japo wakati mwingine wanapingana naye lakini (Matiang’i) akiamua kitu kifanyike basi kitafanyika. Alipokuwa Waziri wa Elimu, Matiang’i alipambana na wezi wa mitihani na pia kubadili mfumo wa utoaji matokeo ambapo sasa wanafuzu wanaomaliza shule za msingi wanapata matokeo mwezi moja baada ya kufanya mitihani.
Rais Uhuru alimteua Matiang’i kukaimu nafasi ya Waziri wa Usalama wa Ndani mwezi moja kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 kutokana na kifo cha Meja Jenerali Mstaafu Joseph Nkaiserry na kwa kushirikiana na polisi, alipambana na waandamanaji waliosababisha vurugu mara tu baada ya Rais Uhuru kutangazwa mshindi.
Ni dhahiri Matiang’i anaonekana kuaminiwa na Rais Uhuru ambaye amedhamiria kuona Serikali yake inatekeleza miradi ya maendeleo. Uteuzi wa Matiang’i umetafsiriwa kurudishwa kwa cheo cha Waziri Mkuu ijapokuwa sio rasmi ukizingatia (Matiang’i) anayo mamlaka kuongoza vikao vya baraza la mawaziri na kuripoti moja kwa moja kwa Rais.
Je, Matiang’i ambaye kiuhalisia si mwanasiasa anaweza akawa anaandaliwa kurithi mikoba ya Rais Uhuru? Ikumbukwe Novemba mwaka jana, Rais Uhuru akiwa ziarani Nyeri kufungua soko la Karatina, alighadhabishwa na viongozi wa eneo hilo ambao wanataka atamke nani atakayemrithi badala ya kujadili mambo ya msingi yanayogusa wananchi wa eneo lao.
“Wengine wanafikiri nimenyamaza kwa sababu siwezi kuongea kuhusu siasa. Mimi bado ni mwanasiasa. Watashangaa chaguo langu muda huo utakapofika, lakini kwa sasa nataka nijihusishe na kutekeleza ahadi nilizotoa kwa Wakenya,” alisema.
Huku wafuasi wa Naibu Rais wakiona kama ni njama za kumuondoa Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022, Ruto mwenyewe ameibuka na kuwakata maofisa wote wa Serikali kutekeleza agizo hilo jipya la Rais.
Ruto ambaye alikuwa na Uhuru wakipata chakula cha mchana jijini Mombasa siku moja baada ya Rais kutoa agizo hilo kuu, inadaiwa alienda kufahamishwa kwanini Rais aliamua kumuongeza majukumu Waziri Matiang’i. Baadaye inaelezwa viongozi hao wawili walikutana na viongozi waandamizi wa Chama cha Jubilee kitendo ambacho kinaonekana ni kuimarisha chama ambacho siku za hivi karibuni kimekuwa katika mgogoro.