Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Januari 11, 2024 amezindua Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini B Pangatupu iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja yenye uwezo wa kuhudumia wananchi zaidi ya laki moja kwenye Shehia 31 wilayani humo.
Akizungumza baada ya ufunguzi wa hospitali hiyo iliyogharimu Sh Bilioni 6.7 Mheshimiwa Majaliwa amesema itasaidia kupunguza adha kwa wakazi wa maeneo hayo kusafiri umbali mrefu kupata huduma za afya.
Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa hospitali hiyo ni utekelezaji wa vitendo wa dhamira ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuhakikisha anawekeza katika sekta ya afya kwa ajili ya ustawi wa jamii.
“Ni dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na maono ya Mheshimiwa Dkt Hussein Mwinyi ya kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma katika mazingira bora na kwa viwango vinavyokubalika,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema kuwa hospitali hiyo itasaidia upatikanaji wa huduma bora za matibabu hususan huduma za kibingwa ambazo hutolewa kuanzia ngazi ya hospitali ya Wilaya. “Miundombinu iliyopo katika hospitali hii, itawezesha kambi za matibabu ya huduma za kibingwa na kibobezi kufanyika hapa kwa mafanikio makubwa badala ya kufanyika katika hospitali za mjini tu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya ifanye tathmini ya kina ya mahitaji ya hospitali hiyo pamoja na kuhakikisha inapangiwa wafanyakazi wa fani zote wanaohitajika kwa mujibu wa kada zao wakiwemo madaktari, wauguzi pamoja na wataalamu wengine.
Pia, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa sekta ya afya waendelee kufanya kazi kwa uadilifu na kujitoa. “Kuwa na majengo na vifaa tiba ni sehemu moja, lakini ubinadamu, upendo na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi ni muhimu katika kuboresha huduma bora kwa wananchi,” amesema.
Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi, idadi ya vitanda vya kulaza wagonjwa vimeongezeka kutoka 1,445 hadi 2,645, idadi ya majengo ya wagonjwa mahututi zimeongezeka kutoka (ICU) moja hadi 14, vyumba vya upasuaji vimeongezeka kutoka 11 hadi 35 kati yake 13 ni kwa ajili ya kina mama pia vitengo vya huduma za dharura vimeongezeka kutoka 2 hadi 13.