30.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AWAONYA VIONGOZI WAPYA SHIRECU

MAFUTA: Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitazama ndoo za mafuta ya kula yaliyokamuliwa  kutokana na mbegu za pamba wakati alipotembelea Kiwanda cha kukamua mafuta ya mbegu cha Jielong kilichopo nje kidogo ya mji wa Shinyanga jana. Kushoto ni Meneja wa kiwanda hicho, Gemin Shao. PICHA: OWM
Na Mwandishi Wetu- Shinyanga             |     

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wapya wa Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (Shirecu), wajipime kama wako tayari kuwatumikia wananchi na kama sivyo waachie ngazi.

Agizo hilo alilitoa mjini hapa juzi wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Mwangongo na vijiji vya jirani baada ya kukagua soko la pamba wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Majaliwa aliyekuwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tano mkoani humo, aliwataka wajumbe hao wajitafakari upya na kujihoji kama wameomba vyeo hivyo kwa ajili ya kupata utajiri ama kuwatumikia wananchi.

“Napenda kusisitiza kwamba ule mfumo wa zamani wa ushirika hivi sasa haupo. Kama uliomba cheo hicho kwa ajili ya kupata utajiri, ni bora ujiondoe sasa hivi, njoo uniambie wakati bado niko kwenye ziara ya mkoa huu, tutatafuta wajumbe wengine ambao ni waaminifu.

“Nasisitiza kwa viongozi wa Amcos na Shirecu, mmeomba vyeo hivyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si kujinufaisha binafsi,” alisisitiza.

Alisema tofauti na ilivyokuwa awali, Serikali inataka kuona ushirika wa sasa ukirejesha matumaini kwa wananchi.

Akitoa mfano, alisema zamani, ushirika ulimwezesha mwananchi kununua baiskeli au redio, lakini kutokana na hali ilivyobadilika, jambo hilo lilikuwa haliwezekani.

“Tunataka ushirika wa sasa ubadilike na umwezeshe mwananchi kununua gari la kutembelea ama kujenga nyumba bora,” alisema.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alisema barabara ya kutoka Kolandoto hadi Igelekelo imeshafanyiwa usanifu na Serikali ya Ujerumani imeanza mazungumzo na Serikali ya Tanzania kuhusu ujenzi wake.

Kwandikwa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi wa Kijiji cha Mwangongo waliokuwa wakisubiri kumsikiliza Majaliwa.

“Kazi ya usanifu wa barabara hiyo imekamilika, tumeanza mazungumzo ya kutafuta wafadhili. Ujenzi wake ukikamilika, utakuwa umerahisisha kuunganisha mkoa huu na mikoa ya Singida, Arusha na Manyara.

“Kutoka Shinyanga hadi Singida tutakuwa tumepunguza kilomita 250, wakati kutoka Shinyanga hadi Karatu tutakuwa tumepunguza kilomita 400 badala ya kupita kwanza Nzega, uende Singida hadi Karatu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles