28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ATAKA TANESCO KUHARAKISHA UMEME RUANGWA

NA MWANDISHI MAALUMU -RUANGWA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemtaka Meneja wa Tanesco Wilaya ya Ruangwa, Samuel Pyuza, ahakikishe umeme unapatikana mapema kwenye pampu ya maji ili kukamilisha mradi wa maji wa Namahema ‘A’.

Ametoa wito huo juzi wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Namahema ‘A’ na Namahema ‘B’ wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, walikofika kumsikiliza mara baada ya kukagua mradi wa maji ambao umechukua miezi sita tangu uanze. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Januari 15, mwakani.

Mradi huo ambao hadi kukamilika kwake utagharimu Sh milioni 244.52, unatarajiwa kuwahudumia wakazi 2,257 wa vijiji hivyo viwili ambao walikuwa wanasongamana kupata maji kutoka kwenye kisima ambacho kilikuwa kinatumia pampu ya mkono. Kijiji cha Namahema ‘A’ kina watu 1,668 na Namahema ‘B’ kina watu 589.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Jumla ya Sh milioni 189.93 zimeshatumika kwenye mradi huo ambazo ni sawa na asilimia 77.68 ya fedha zilizopangwa kutumika. Fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Maji wa Taifa (National Water Investment Fund).

Kazi ambazo zimekamilika hadi sasa ni ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DP) 32, ujenzi wa mtandao wa mabomba yenye urefu wa mita 6,460, tenki la kuhifadhia maji leye ujazo wa lita 50,000, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house), ujenzi wa uzio (fence) kwenye nyumba ya mitambo, ujenzi wa uzio (fence) kwenye tenki la kuhifadhia maji na ununuzi wa pampu na mota.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles