Na MWANDISHI WETU -DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mawaziri na naibu mawaziri wao wajiepushe kutoa matamshi yasiyotekelezeka kuepuka mkanganyiko serikalini.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akifungua kikao kazi cha mawaziri kwenye ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma.
Alisema ni vema viongozi hao kabla ya kutoa matamko wakajiridhisha iwapo jambo hilo halitaleta athari za bajeti na sera na kama lipo katika bajeti za wizara zao.
Pia amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi kuithibitishia jamii kuwa Rais Dk. John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao katika utendaji.
“Tunao wajibu mkubwa kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii kutimiza matarajio ya Rais Dk. Magufuli na wananchi wote kwa ujumla,” alisema
Aliwataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
Pia amewataka wafuatilie na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa wao ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Waziri Mkuu amesema mawaziri na naibu mawaziri wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.
Pia wasimamie utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na ahadi alizozitoa Rais Dk. Magufuli, wakati wa kampeni za uchaguzi.