RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, ya kutaka kutengua uamuzi wa kuvuliwa ubunge na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Uamuzi huo ulitolewa jijini hapa jana na Jaji Latifa Mansour.
Katika uamuzi wake alioutoa kwa dakika 44, Jaji Mansour, alisema analiondoa shauri hilo mahakamani kwa vile Ndugai alifanya hivyo kutokana na kanuni za Bunge zinavyoelekeza kuwa mbunge asipohudhuria vikao vitatu mfululizo atakuwa amepoteza sifa za kuwa mbunge.
“Shauri hili linaondolewa mahakamani kwa sababu Spika alifanya uamuzi kulingana na kanuni za Bunge zinavyoelekeza,” alisema.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili wa Nassari, Fred Kalonga, alisema mahakama inasema Spika alifanya uamuzi sahihi hivyo wanaenda kukaa na kujadiliana na mawakili wenzake kutafuta tafsiri zaidi.
“Mahakama inasema Spika alifanya uamuzi ndiyo maana shauri hilo limeondolewa, tutakwenda kutafakari na mawakili wenzangu na tutakwenda kutafuta tafsiri zaidi katika mahakama ya rufani,” alisema.
NASSARI
Akizungumza nje ya mahakama baada ya hukumu hiyo, Nassari, alisema hilo ni jambo la kawaida kwake na wala hatishiki na anamwachia Mungu.
Pia alisema siku zote dhahabu haiwezi kung’aa hadi ipitie katika moto.
“Kufanya mageuzi kwenye nchi za Afrika si kazi rahisi, tulianguka na ndege tukapona, niliwahi kuvamiwa na majambazi nyumbani kwangu wakaambulia kuua mbwa, hili ni jambo dogo ambalo haliwezi kuniondolea uhai,” alisema.
Machi 27, mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mawakili wa pande mbili walivutana kuhusu kanuni ya kudumu ya Bunge kifungu namba 146 (3) kilichomvua ubunge Nassari.
Mvutano huo uliibuka baada ya upande wa Jamhuri kudai Ndugai yupo sahihi huku upande wa utetezi ukidai kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni hiyo.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili, Alesia Mbuya na Masunga Kawahanga, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Pius Mboya kutoka Ofisi ya Bunge.
Upande wa utetezi ulikuwa na mawakili, Hekima Mwasipu na Fred Kalonga.
Wakili Mbuya alidai Spika yupo sahihi katika uamuzi wake kwa kuwa kanuni inasema mbunge atakoma ubunge asipohudhuria mfululizo bila taarifa mikutano mitatu ya Bunge.
Naye Wakili Kalonga alidai kabla ya kufikia uamuzi huo, Spika, alipaswa kutoa onyo kama kanuni inavyoelekeza lakini hakufanya hivyo na kudai kuwa amekiuka kanuni katika uamuzi wake.
Machi 20, mwaka huu, mahakama hiyo ilizuia kutofanyika uchaguzi wa Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki hadi shauri la kutoridhishwa na uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge Nassari litakapoamuriwa.
Katika kesi hiyo, Nassari, aliomba kibali cha kufungua kesi ya msingi kwa ajili ya kutengua uamuzi wa Spika.
Machi 14, mwaka huu, Ndugai alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki linaloongozwa na Nassari lipo wazi baada ya kupoteza sifa ya kuwa mbunge.
Barua hiyo ilieleza kuwa Nassari amepoteza sifa ya kuwa mbunge kutokana na kitendo chake cha kutohudhuria mfululizo vikao vitatu vya mikutano ya Bunge ambao ni mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, mwaka jana, mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, mwaka jana na mkutano wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9, mwaka huu.
Uamuzi wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Tanzania ibara ya 71 (1) (c).
Ibara hiyo inaeleza kuwa mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila ya ruhusa ya Spika.
Ibara hiyo pia imefafanua katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo ya Januari, 2016 kuwa kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano mitatu mfululizo ya Bunge bila ruhusa ya spika iliyotolewa kwa maandishi atapoteza ubunge wake na spika ataiarifu NEC.