Na Mwandishi Wetu, Kigoma
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Kigoma, imetoa amri kwa Bodi ya Wadhamini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadaiwa wengine kusitisha shughuli zote katika eneo lenye mgogoro kati yao na Kanisa Katoliki wilayani Uvinza.
Amri hiyo ya Mahakama ilitolewa Februari 15, 2023 mbele ya Jaji Mfawidhi, Lameck Mlacha baada ya muombaji Kanisa Katoliki Jimbo la Kigoma kuwasilisha maombi chini ya hati ya dharura wakidai ni wamiliki halali wa eneo hilo lililopo eneo la Nyambutwe, wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Mleta maombi katika shauri hilo anawakilishwa na Wakili Method Kabuguzi akishirikiana na Wakili Mgaya Mtaki na wajibu maombi wanawakilishwa na Wakili Fabian Donatus na Hamis Kimilomilo huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili Allan Shija.
Waombaji katika shauri hilo wanadai mjibu maombi namba mbili, Wizara na Halmashauri ya Uvinza wamepanga kuchukua eneo lao kuwapa CCM bila ridhaa yao kwa ajili ya kujenga madarasa ya Shule ya Sekondari ya Chumvi.
Kanisa Katoliki waliiomba Mahakama ikubali kutoa amri ya zuio la muda kwa wajibu maombi na mawakala wao au watu wengine kujenga au kuendeleza eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 39.6.
Baada ya kusikiliza maombi hayo Mahakama iliyakubali na kutoa amri tatu kwamba kuanzia jana CCM na wengine wote kwenye eneo lenye mgogoro hawaruhusiwi kujenga ama kuendeleza kitu chochote mpaka kesi itakaposikilizwa na kuamriwa.
Mahakama imezuia upande wa Serikali kufanya ama kuendelea na upimaji katika eneo lenye mgogoro.
Pia Serikali hairuhusiwi kufanya ugawaji ama umilikishaji wowote kwenye eneo lenye mgogoro.
Upande wa Serikali uliwasilisha majibu ya madai yanayowakabili lakini CCM walikuwa hawana majibu yoyote waliomba wapewe muda, hivyo Mahakama iliwaamuru kuwasilisha majibu yao ndani ya siku saba.
Awali Wakili wa CCM, Fabian Donatus alidai nyaraka zilihifadhiwa katika Ofisi ya Kigoma na kwa bahati mbaya zilichelewa kuwafikia Dodoma hivyo wakaomba siku saba ili kuweza kuwasilisha majibu ya kiapo kinzani na kuendelea na kesi hiyo.
Wakili wa Mleta maombi, Mgaya Mtaki alidai ni haki yao ya msingi kuwasilisha hati ya kiapo kinzani mahakamani hapo na kwamba wao hawana pingamizi.
Shauri limepangwa kuendelea Machi 3 mwaka huu.
Shauri hilo liliwasilishwa chini ya hati ya dharura na kupewa namba 42/2022 dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya CCM, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.