NA OMARY MLEKWA-MWANGA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro imeamuru ng’ombe 1,325 waliokamatwa katika operesheni ya kukamata mifugo inayoingizwa nchini kinyume na taratibu kwa ajili ya malisho, kupigwa mnada Oktoba 20, mwaka huu.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema licha ya mifugo hiyo kuingizwa nchini pia imechangia uharibifu wa mazingira, kukauka vyanzo vya maji, uharibifu wa misitu na mmomonyoko wa udongo.
Aliyasema hayo alipotembelea eneo la Kata ya Mgagao walipohifadhiwa ng’ombe hao
Mpina alisema operesheni inayoendelea ya kusaka mifugo iliyoingia nchini kinyume cha sheria isihusishwe na ushirikiano mwema uliopo baina ya Tanzania na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Mahakama imeiteua na kutoa idhini kwa Kampuni ya Maripelanto Auctioneer & Court Broker ya Moshi kusimamia uuzwaji wa ng’ombe hao keshokutwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo alilolitoa wiki iliyopita la kutaka mifugo hiyo itaifishwe.
“Tunafanya operesheni hiyo ya kwanza na ya mwisho kwa sababu haiwezekani makundi makubwa ya mifugo yakaingia nchini wakati maeneo hayo wapo watumishi wa Serikali.
“Hivyo ni dhahiri kutakuwa na uwajibikaji hafifu wa watumishi hao na kamwe Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli haitawavumilia watumishi wa aina hiyo,” alisema Mpina.
Alisema muda wa siku saba aliotoa wa mifugo kuondolewa nchini umekwisha na ataongoza operesheni nchi nzima itakayochukua siku 15 kuhakikisha hakuna mfugo hata mmoja utakaobaki kutoka nchi jirani.
“Tanzania haiwezi kuwa mahali pa kulisha mifugo kutoka nchi jirani huku wafugaji wazawa wakiendelea kuteseka kwa kukosa malisho.
“Inakadiriwa kuwa asilimia 30 ya malisho yanatumiwa na mifugo kutoka nje ya nchi ambako Sheria ya Mifugo Namba 17 ya Mwaka 2003 inakataza mifugo kuingia nchini bila kibali,” alisema .
Waziri alisema hatua hizo kali anazozichukua sasa zimelenga kuwakinga wafugaji wazawa na magonjwa ya mifugo kutoka nje ya nchi kwa sababu ikiwa hali hiyo itaendelea ng’ombe wengi watakufa huku Serikali ikilazimika kutumia gharama kubwa kutibu mifugo hiyo.
Mpina amewaagiza wakuu wote wa mikoa na wilaya za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mara, Kagera, Tanga, Songwe, Mbeya, Katavi, Njombe, Kigoma kusimamia hatua hiyo ya mifugo kurudishwa nchi zilikotoka.
Alisema hicho ndicho kitakuwa kipimo cha viongozi hao katika kusimamia shughuli za Serikali.
“Katibu Mkuu wa wizara na maofisa mifugo kote nchini hakikisheni mnasimamia kwa ukamilifu sheria na katika kipindi hiki cha mimi kuwa waziri wa wizara hii na Serikali ya awamu ya tano hatimaye mifugo na mazao yake viweze kuleta tija kwa Taifa,”alisema Mpina.
Mambo ya Nje wanena
Wizara ya Mambo ya Nje Na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imetoa tamko na la uingizaji mifugo kutoka nchi moja kwenda nyingine ikisema una madhara mengi, yakiwamo ya usalama, uharibifu wa mazingira na kueneza magonjwa ya mifugo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Oktoba 13, mwaka huu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitoa agizo la kuondoa mifugo yote iliyopo nchini kinyume cha sheria ndani ya siku saba na kutofanya hivyo kutasababisha mifugo hiyo kutaifishwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inatoa wito kwa Watanzania wote wenye mifugo nchi jirani wafuate taratibu za sheria na kama kuna mifugo kwenye malisho nje ya Tanzania waiondoe mara moja kuepusha hasara na usumbufu,” ilieleza taarifa hiyo