28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Pinda ni wa tofauti

*Aeleza sababu za kumwakilisha mkutano China

MWANDISHI WETU-KATAVI

RAIS Dk. John Magufuli amesema Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ni wa tofauti kwani amekuwa ni miongoni mwa viongozi wastaafu wanaomsaidia kuongoza nchi.

Alitoa kauli hiyo jana mkoani Katavi wakati akizindua Barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni yenye urefu wa kilomita 76.6.

“Leo hapa (jana) tungekuwa na Mizengo Pinda, lakini nimemtuma China ili akaniwakilishe katika kuadhimisha miaka 20 ya Mwalimu Nyerere.

“Niliona hakuna mwingine ambaye angewakilisha vizuri, nikasema ni Pinda Mizengo Pinda ndiyo aende, kwa hiyo ndiyo maana hapa hamjamwona.

“Pinda ni mtu mwema sana, ananisaidia sana katika kazi, ni baba mwenye moyo wa tofauti sana na ndiyo maana nimemchagua kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ananisaidia kuongoza nchi na chama kwa ushauri katika mambo mbalimbali, kwa sababu ni mtu mmoja mstaarabu sana.

 “Na ndiyo maana nimemtuma China akaniwakilishe katika maadhimisho ya miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere. Niliona sina mwingine wa kumtuma atakayeniwakilisha vizuri, nikasema Mizengo Pinda ndio aende, ni baba mwenye moyo wa tofauti,” alisema Magufuli.

Pinda amekuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Edward Lowassa.

AGAWA MAPORI

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwapa maeneo wananchi wa Mkoa wa Katavi, vijiji 60 kati ya 920 vya nchi nzima ambavyo vilikuwa kwenye mapori tengefu pamoja na hifadhi za taifa ili waweze kujishughulisha na kilimo, ufugaji na kufanya makazi.

Hatua hiyo imetokana na Serikali kuunda kamati ya mawaziri nane kufanya uchunguzi kuhusu migogoro iliyoko kwenye mipaka nchi nzima.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema wakati nchi inapata uhuru mwaka 1961, ilikuwa ikikaliwa na wananchi milioni tisa pekee sambamba na mifugo milioni 38.5.

Rais Magufuli alisema ongezeko la watu hao pamoja na mifugo ni lazima wananchi hao wapewe baadhi ya maeneo ili waweze kumudu shughuli zao.

“Nawapatia maeneo haya, hakuna mtu yeyote wa kuwatoa, mtakaa hapa hapa maisha yenu yote na hakuna mtu yeyote yule atakayeweza pia kuja kubomoa nyumba zenu hata kama ni choo,” alisema.

Kutokana na hilo, alimwagiza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi kuhakikisha maeneo yote ya vijiji yaliyokuwa ndani ya mapori tengefu na hifadhi wanayapima na kuweka alama.

 “Mkifanya hivyo kama ambavyo Tanroad wamekuwa wakifanya kwenye mipaka ya barabara zao, itasaidia kuondoa migongano kati ya wananchi na Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu na Wanyama,” alisema.

Alisema lengo la Serikali ni kuifanya Hifadhi  ya Katavi kuwa ya kimataifa ili iweze kukuza uchumi zaidi wa mkoa, kwa sababu watalii wamezoea kwenda zaidi kwenye hifadhi za mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. 

Vilevile Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe afanye upembuzi yakinifu barabara yenye urefu wa kilomita 71 kutoka Kibaoni hadi Stalike ili kuunganisha na barabara kutoka Mpanda hadi Stalike.

“Hii itafanya Mkoa wa Katavi na Rukwa kuwa na barabara yenye viwango vya lami tofauti na ilivyo sasa ambapo barabara hiyo ina kilomita 71 ya changarawe,” alisema.

Alisisitiza kuwa uwezo wa Serikali kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami upo kwani itatumia fedha zinazorudishwa na mafisadi kutekeleza miradi ya ujenzi ya barabara.

Kwa upande wake, Lukuvi alivitaja baadhi ya vijiji ambavyo wananchi wa Mkoa wa Katavi wamepewa maeneo na Rais Magufuli ni Mapili, Nsenkwa, Kamalampaka, Masigo, Mgombe pamoja na Uzega.

Vingine ni Mwamapuli, Ukingwamize, Ikuba, Majimoto, Usevya, Masigo, Lubwaga, Utende, Ilunde, Mgombe, Mtakuja, Stalike pamoja na Kaloleni.

AGIZO TANAPA

Akiwa njiani kutoka Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa kuelekea Mpanda mkoani Katavi, Rais Magufuli alisalimiana na wananchi wa Kizi (Nkasi) na Mirumba (Mlele) na baadaye wananchi wa Stalike wilayani Mpanda na amewahakikishia kuwa vitongoji vya Igalukilo, Kabenga, Kaloleni na Situbwike havitaondolewa katika maeneo ya hifadhi kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuvirasimisha.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli alitembelea Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kisha kuzungumza na maofisa na askari Wanyamapori wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), ambapo amewapongeza kwa kazi nzuri ya kuhifadhi wanyamapori ikiwemo kukabiliana na ujangili hali iliyowezesha kuongezeka kwa idadi ya wanyama wakiwemo wale waliokuwa hatarini kutoweka.

Alimtaka Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk. Allan Kijazi kuchimba mabwawa ya kuvuna maji mengi zaidi ya mvua yatakayowasaidia wanyama, hasa viboko wakati wa kiangazi kikali pamoja na kujipanga kuzuia wanyama wakali wanaoweza kuvamia makazi ya watu na kuhatarisha maisha ya wananchi.

Rais Magufuli ambaye ameambatana na mke wake Janeth, leo ataendelea na ziara yake mkoani Katavi ambako ataweka jiwe la msingi katika miradi ya njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilowati 132 kutoka Tabora hadi Mpanda, Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika na barabara ya lami ya Mpanda – Vikonge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles