29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli amtaka Museveni kuwa mkali

Elizabeth Hombo Na Asha Bani -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amemtaka Rais wa Uganda, Yoweri Museveni wa Uganda kuwa mkali kwa watendaji, ili kuhakikisha mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga, unatekelezwa kwa wakati, tofauti na sasa ambapo unasuasua.

Aliyasema hayo jana wakati akifungua kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda, jijini Dar es Salaam jana, ambapo yeye na Museveni walikuwa wageni rasmi. 

Kutokana na hilo, amesema anatamani watendaji wa Tanzania wangeenda Uganda na wa Uganda waje Tanzania ili ashughulike nao angalau kwa mwezi mmoja tu.

Alisema yeye tangu aingia madarakani mwaka 2015, ameshabadilisha makamishna wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watano lengo likiwa ni kuleta mabadiliko katika mamlaka hiyo.

 “Nilikuwa namwuliza mzee Museveni mbona unachelewesha hili bomba, kwa sababu ya kodi ya huko ambayo umekataa kuikubali ya dola 600 wakati utakuwa unatengeneza dola bilioni 800, jitolee hii kodi kidogo utengeneze ajira na utakuwa unapata fedha.

“Kwa muda mrefu watu wako wa URA yaani Uganda Revenue Authority wamekuwa wakikuchelewesha, sisi tulitaka hilo bomba liitwe Kaguta Pipeline siku tunapozindua, hao wasikucheleweshe.

“Nikamtolea mfano Museveni kuwa nilipoingia madarakani tayari nimebadilisha makamshina watano wa TRA, si suala la kujidai ni baya, lakini nikamwambia wewe umemg’ang’ania wa nini huko? Tunatakiwa tusonge mbele kibiashara.

“Imebidi tulizungumze hili maana mimi linaniuma, tulibidi tupeleke mabadiliko ya sheria ya kodi ili hili bomba lijengwe, sisi Tanzania mikoa minane itafaidika na hili bomba likishaanza collection ya revenue (makusanyo ya kodi) ya Uganda itakuwa ndiyo inaongoza katika uchumi wa bara la Afrika sasa kwanini ucheleweshwe na watendaji?

“I wish (ninatamani) hawa watendaji wa Tanzania wangeenda Uganda na wa Uganda waje Tanzania ili ni-deal (nishughulike) nao angalau kwa mwezi mmoja tu,” alisema Rais Magufuli.

Magufuli aliwataka watendaji katika nchi za Uganda na Tanzania wahakikishe wanafanikisha miradi mikubwa ambayo inatengeneza ajira nyingi.

Alisema ana imani kupitia kongamano hilo, wafanyabiashara hao kutoka Uganda na Tanzania watatoka na majibu kuhusu masuala ambayo yamekuwa yakikwamisha biashara katika nchi hizo.

Kwa upande wake, Rais Museveni alimhakikishia Rais Magufuli kwamba Serikali yake itahakikisha bomba hilo la mafuta linajengwa na mafuta ambayo yamekuwepo kwa miaka milioni mbili iliyopita yanapatikana kwa maendeleo ya wananchi.

Vilevile aliwataka wafanyabiashara hao kujadiliana kwa kina na kujibu swali linalouliza ‘utajiri wa mataifa unatoka wapi?’ kama lilivyoulizwa na Adam Smith kwenye kitabu chake cha Wealth of Nations (Utajiri wa Mataifa).

Rais Museveni alisema suala la miundombinu ni muhimu katika kurahisisha biashara baina ya mataifa hayo, kwa sababu gharama za usafirishaji wa kontena kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Port Berry kwa reli na bandari itakuwa dola za Kimarekani 1,600 badala ya dola 4,500 za sasa.

Awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Salum Shamte, alisema Tanzania na Uganda zimekuwa zikifanya biashara kwa muda mrefu lakini biashara hiyo inaweza kuongezeka zaidi ya sasa.

Alisema Serikali inachukua hatua mbalimbali kuboresha mazingira ya biashara na wao wanashirikishwa kikamilifu.

 “Tunaomba muendelee kuboresha mazingira ya biashara na kutuhusisha kwenye miradi mikubwa kama ule wa bomba la mafuta kutoka Hoima mpaka Tanga. Tunaahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo,” alisema Shamte.

Naye mjumbe wa Bodi ya Sekta Binafsi ya Uganda, Mariana Sabune, alisema biashara kati ya nchi hizo mbili inakabiliwa na changamoto ya vikwazo visivyo vya kikodi ambavyo vimewekwa na nchi husika.

Alisema vikwazo hivyo vimekuwa vikitatiza shughuli za biashara baina ya Tanzania na Uganda na endapo vitaondolewa, wafanyabiashara watafanya shughuli zao kwa ukamilifu bila vikwazo vyovyote.

“Nampongeza Rais Magufuli kwa kuibadilisha sheria ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA), tunaamini kwamba mabadiliko hayo yataondoa vikwazo visivyo vya kikodi,” alisema Sebune.

Alisema makubaliano ambayo yanafikiwa kwenye mikutano ya tume ya pamoja ya kudumu na sekta binafsi yawe yanafanyiwa kazi na kufuatiliwa kwa sababu wamekuwa wakifanya mikutano mingi lakini hakuna utekelezaji wowote.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema ana Imani kongamano hilo litakuja na maazimio au hatua ya namna ya kukuza uwekezaji katika nchi hizo mbili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles