25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

MADUDU MFUMO WA ELIMU YACHAMBULIWA

Profesa Kitila Mkumbo
Profesa Kitila Mkumbo

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

WATAALAMU wa elimu nchini wamechambua changamoto zilizopo ikiwamo kiwango duni cha mfumo uliopo sasa.

Kutokana na hali hiyo, wamesema mfumo uliopo sasa unashindwa kuandaa vijana katika soko la ajira, huku wataalamu waliopo vyuoni wakipewa kazi nyingine serikalini na nafasi zao zikiendelea kuwa wazi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mhadhiri wa Chuo Kikuu kishiriki cha Elimu (DUCE) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akiwasilisha mada katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa HakiElimu 2017-2010.

Profesa Kitila alisema mfumo wa sasa wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi chuo kikuu hauko vizuri, kwamba kwa sasa elimu imebaki bila kuwa na njia mbadala ya kuiboresha zaidi ili kuweza kwenda na mabadiliko ya dunia.

“Tunaposema elimu ni lazima tuandae ‘Global Citizen’, kwa sasa kitu hicho hatuna hapa kwetu. Sasa sekta ya elimu inakabiliwa na changamoto, kiwango duni cha elimu inayotolewa, mfumo wa elimu hauwapi uelewa (skills) wahitimu na kwa upande wa elimu ya juu hawajajipanga vyema.

“Elimu ya juu wanaofundisha wengi hawana sifa ya kufundisha elimu ya juu, ni robo tu wenye sifa ya kufundisha na kwamba asilimia 41 ndio wenye Phd, lakini wengine hawana.

“Tunahitaji wenye Phd wanaofundisha vyuoni angalau wafikie asilimia 60 na kuna haja ya kuishawishi Serikali kuwekeza katika elimu. Walimu ni tatizo kubwa, Serikali inatakiwa kuwaangalia na kuwapa mafunzo kwani mafunzo ni muhimu na ni jambo endelevu,” alisema Prof. Kitila.

Akizungumzia mpango huo mkakati, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalage, alisema maeneo yaliyolengwa ni kushawishi mabadiliko ya sera kupitia ufumbuzi unaozingatia ushahidi, kufuatilia utekelezaji wa sera na kudai kutetea mageuzi.

Pia umelenga kukuza ushiriki wa jamii kupitia kuwapa taarifa wananchi, kutoa fursa kwa wananchi kushiriki masuala ya kijamii na kukuza uwazi na uwajibikaji kwa kudai uwazi kwenye bajeti na kukua usikivu na uwajibikaji wa Serikali.

“Uwazi na uwajibikaji ni mambo muhimu kwenye utawala wa kidemokrasia, uwazi wa Serikali unawawezesha walipa kodi kutafiti na kujua kiurahisi utendaji wa Serikali na kuiwajibisha Serikali au viongozi wa kuchaguliwa kutokana na jinsi wanavyotumia fedha za walipakodi kwenye ngazi zote,” alisema.

Akizungumzia shule tisa zilizofanya vibaya matokeo ya kidato cha pili Mkoa wa Mtwara, alisema wazazi wanachangia kufanya vibaya wanafunzi katika mitihani mkoani humo.

Katika mpango mkakati huo, ilielezwa kuwa mambo yanayochangia kudorora kwa elimu ni pamoja na kupata matokeo duni ya kujifunza kwa wanafunzi, utoro wa walimu na umahiri duni wa kufundisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles