Na MALIMA LUBASHA-SERENGETI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Serengeti mkoani Mara, imewataka madiwani kuwafichua watendaji na wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya kiwango huku wakiwa wamepokea fedha.
Onyo hilo limetolewa na Kamanda wa Takukuru wa Wilaya ya Serengeti, Emmanuel Lihuda, katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, baada ya Diwani wa Kata ya Rigicha, Eliya Limbu, kulalamika miradi mingi inayotekelezwa wilayani iko chini ya kiwango huku Takukuru wakishindwa kuwachukulia hatua wahusika.
Aliwataka madiwani hao wasisite kuwafichua watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo vya kuhujumu miradi ya halmashauri na kuwataka kutoa ushirikiano kwa chombo hicho wanapobaini kasoro katika utekelezaji wa miradi huko vijijini kwenye kata zao ambayo iko chini ya kiwango na wapo tayari kuchukua hatua.
“Takukuru tukipata fununu kwamba kuna matumizi hewa katika miradi ya ujenzi wa barabara, maji, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa fedha za miradi na kwamba wapo watendaji wanashirikiana na wakandarasi kuhujumu miradi tutawakamata, kuwahoji na kuwafikisha mahakamani,” alisema Lihuda.
Alisema kila mara anapita vijijini kutoa elimu dhidi ya vitendo vya rushwa kwa jamii na kuwataka kuwajata wanaojihusisha na kuwataka madiwani kuendelea kutoa taarifa wanapobaini kuna mazingira ya rushwa na wao wawe mfano kukataa kupokea ama kutoa rushwa katika kutoa tenda za zabuni.
Diwani Limbu, akijadili taarifa hiyo ya uwajibikaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kipindi cha 2016/2017, alilalamika kuwa miradi mingi huko vijijini inatekelezwa chini ya kiwango na fedha za Serikali zinapotea bure huku taasisi ikikaa kimya bila kuchukua hatua yoyote kwa wahusika
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Nestory Jonas, aliahidi kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kuhusu taarifa hiyo na kuhakikisha fedha zinapelekwa kwa wakati kutekeleza miradi huko vijijini.