Na WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM
MTAALAMU wa masuala ya fiziotherapia wa idara ya kina mama katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Elieka Kaaya ameeleza madhara saba ya ufungaji tumbo baada ya kujifungua, ikiwa ni pamoja na kupunguza mfumo wa upumuaji na mzunguko wa damu chini ya miguu.
Akizungumza na MTANZANIA wakati wa mahojino maalumu Dar es Salaam jana, Dk. Kaaya alisema madhara ya ufungaji tumbo baada ya kujifungua ni mengi kuliko faida, hivyo kuna haja kina mama kupata ushauri wa wataalamu wa afya ya uzazi.
“Kwenye ufungaji wa matumbo hasara zinakuwa nyingi kuliko faida ambayo ni kurudisha misuli ya tumbo katika hali ya kawaida, ingawa baada ya muda unakuwa umeharibu misuli ya ndani.
“Hasara mojawapo ni kupunguza mfumo wa upumuji kwa sababu kuna msuli unaitwa ‘diaphragm’ ambao uko juu ya tumbo, huu una asilimia 60 ya mwanadamu kupumua, utakapokuwa umefunga unaweza kukuzuia kupumua vizuri (shallow breathing).
“Hasara nyingine ni misuli ya tumbo kukosa nguvu baada ya kulegea na kupunguza ufanyaji kazi kwa ufanisi kwa sababu misuli ya tumbo haijaumbwa ifungwe, iliumbwa iwe imara kubebea pingili mgongo,” alisema Dk. Kaaya.
Alisema hasara nyingine ni kuzuia mzunguko wa damu chini ya miguu na unasababisha uvimbaji wa miguu hali inayosababisha mgando wa damu mwilini unaoweza kuwa na hatari hata kusababisha kifo.
Dk. Kaaya alisema kina mama wanaojifungua kwa njia ya upasuaji wakianza kufunga tumbo kabla ya muda wanaweza kupata ugonjwa wa ngiri (Hernia) kutokana na upasuaji kutokupona na ubanwaji wa misuli.
“Athari nyingine hautakuwa huru na mwili wako na pia kuongeza kutokwa damu kwa kasi kwa sababu ya kuendelea kukandamiza kizazi ambako unasababisha wewe mwenyewe.
“Pia kuna madhara kwenye ngozi kama vipele na kupoteza maji mengi na kumbuka kuwa bado mama huyu huyu ananyonyesha kwahiyo anaweza kupungukiwa na maji mwilini (dehydration),” alibainisha Dk. Kaaya.
Alisema kuwa sababu kubwa ya kina mama kulalamikia maumivu ya mgongo na ganzi ni ufungaji wa tumbo usiofuata ushauri wa wataalamu.
“Mama anayebeba ujauzito anakuwa na homoni anazoachia zinazoruhusu misuli kutanuka ili mtoto akue na pingili za mgongo lazima ziruhusu tumbo kuwa kubwa na kubeba mtoto,” alisema Dk. Kaaya.
Alibainisha faida za ufungaji tumbo kuwa ni misuli kusinyaa na tumbo kurudi katika hali yake ya kawaida.
“Faida za ufungaji tumbo ni chache sana, mojawapo inamhusu mwanamke ambaye kabla ya ujauzito alikuwa na matatizo ya mgongo.
“Tunaweza kumwambia afunge tumbo na kuna utofauti katika ufungaji, hivyo ni vyema kuonana na mtaalamu wa afya ili amwelekeze namna sahihi ya ufungaji wa tumbo.
“Pia inasaidia mama kuzuia pingili za mgongo kutokufyatuka kutokana na misuli kukosa nguvu baada ya kubeba uzito kwa muda mrefu.
“Kwa mtu anayekuwa na mafuta mengi, akibana mafuta yanapungua kwa kiasi fulani ila haipunguzi tumbo kwa asilimia zote, ni lazima kufanya mazoezi baada ya kuelekezwa na mtaalamu kulingana na mwili wake,” alisema Dk. Kaaya.
Alitoa ushauri kwa kina mama wanapojifungua badala ya kufunga mikanda au kanga wafanye mazoezi ya tumbo ambayo wataelekezwa na wataalamu wa afya.