25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Machungu ya kodi mpya kuanza leo

Dk. Philip Mpango
Dk. Philip Mpango

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MACHUNGU ya kodi mpya za Serikali yataanza leo baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 29.5 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Bajeti hiyo iliyowasilishwa Juni 9, mwaka huu bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ilieleza kuanza kukata ushuru wa vinywaji baridi, maji ya juisi, vinywaji vikali, bia na sigara kuanzia Julai Mosi mwaka huu, mwaka wa fedha wa Serikali.

Katika bajeti hiyo ya Serikali ambayo ni ongezeko la Sh trilioni 7 ikilinganishwa na ile ya mwaka wa fedha uliopita, Serikali imepanga kutumia Sh trilioni 17.72 kwa matumizi ya kawaida huku trilioni 11.82 zikiwa zimepangwa kutumika katika matumizi ya maendeleo, ambapo Sh trilioni 8.7 ni fedha za ndani na trilioni 3.1 ni za nje.

Bajeti hiyo itakwenda sambamba na utozaji kodi ambao utawagusa watu wanaotumia huduma za M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, Ezypesa pamoja na wale wanaochukua fedha kwa njia ya mashine za benki (ATM).

Awali kodi ya bidhaa ilikuwa asilimia 10 lakini kwa hatua ya kuongezwa kwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kodi itapaa na kufikia asilimia 18.

Kutokana na hali hiyo kodi ya VAT hulipwa na mtumiaji wa mwisho ambaye anatumia au kupokea huduma, hali ambayo inatajwa kuwaumiza watumiaji wa mwisho ambapo pia yatamgusa mtumiaji wa ATM.

Akizungumza na MTANZANIA, Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Semboja Haji alisema benki pamoja na zile kampuni za simu zitatumia ujanja kwamba wanaopaswa kulipa gharama hizo ni mlaji.

Alisema watatumia ujanja huo kwa sababu haikuwekwa sheria katika tozo hizo mpya kwamba mlaji na kampuni hizo wachangie kidogo .

“Tangu mwanzo wananchi kwa kutumia taasisi zao walitakiwa kulalamika kwamba mzigo kwa mlaji ni mkubwa, kwa kuwa tumeshachelewa iwe tu pendekezo kwamba makato haya yawaguse walaji na kampuni…ilipaswa iwekwe kwenye sheria mapema kwa sababu sasa tafsiri ya kampuni hizi watasema anayepaswa kulipa ni mlaji,”alisema Profesa Semboja.

Kutokana na hilo, gazeti hili lilimtafuta Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungi ili aweze kuzungumzia kuhusu tozo hizo ambapo alisema: “Tozo za shughuli za kibenki husimamiwa na BoT. Zipo kwa mujibu wa Financial Regulation (Kanuni za Fedha). TCRA haisimamii masuala ya fedha,”alisema Mungy.

Alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alimtaka mwandishi habari hii kuzungumza na Hazina au TRA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles