MWANDISHI WETU
HILI litakuwa ni moja ya tukio kubwa la kisiasa kutokea nchini Tanzania. Kama ni tsunami basi ni mama wa tsunami zote za siasa ambazo zimewahi kutokea. Lakini kwani Tanzania kumewahi kuwa na tsunami za kisiasa. Kama zimewahi basi CUF ni sehemu yake muda wote.
Chama cha Wananchi (CUF) kimezoea kufanya au kuandika historia. Ni chama ambacho kwa tafsiri ya wengi ndio mwamba, ndio bingwa na ndio kiboko ya vyama vyote vya siasa nchini Tanzania kwa maana kubwa na pana.
CUF kwa muda wote hadi tukio hili la sasa ndio ambayo imejaribu bila kuogopa, imethubutu bila ya hofu na imejipima bila ya kizuizi katika pirika, harakati na vikwazo mbalimbali ambavyo imewekewa mara tu baada ya kuundwa kwake mwaka 1992 baada ya kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
CUF imekuwa ndio mwamba na nguzo ya vyama vyote vya siasa Tanzania pamoja na kuwa eneo lake la kujidai ni Zanzibar lakini imekuwa na ushawishi mkubwa Bara kama usemavyo ule msemo kuwa “Ikipigwa zumari Zanzibar kwenye maziwa wanacheza,”
Hakuna chama chochote cha siasa ambacho hakikuwa au kisingependa kuungwa mkono na CUF ili kihalalisha afya na uzima wake pamoja na kuwa CUF imekuwa ikiungwa mkono zaidi Zanzibar lakini ikajenga ushawishi mkubwa ambao wote wa Bara na mikoa mingine kadhaa kama Tabora, Ruvuma, Kigoma na baadhi yake.
Shutuma za ugaidi, udini na ukanda zilikiandama chama hicho kwa muda wote, njama za kukihujumu zikapangwa katika kila ofisi nyingine kubwa na nyingine ndogo kikitiwa hila na makosa chama hicho pamoja na viongozi wake kadhaa. Hatari kabisa. Lakini bila mafanikio.
CUF hiyo ikaanza maajabu katika uchaguzi wake wa kwanza wa mwaka 1995 miaka mitatu tu tangu kuundwa na chupuchupu ichukue Serikali ya Zanzibar. Ni kama vile ilijichongea maana kuanzia hapo yaani mwaka 2000, 2005, 2010 na hata 2015 CUF inadai kupokwa ushindi.
Ila yale ya 2015 yalikuwa ndio ya wazi kuliko yote ambapo CUF inaamini kuwa ilishinda kwa tofauti ya kura 25,836 dhidi ya CCM lakini bado ikadai kupokwa ushindi. Na kwa mara ya kwanza ikafikisha wabunge kumi wa majimbo huko Tanzania Bara.
Kwa hiyo kukawa na mwelekeo kuwa CUF sasa inaelekea kufanya makubwa zaidi katika siasa za Tanzania na wazee wa mikakati, wengi tunaamini, wakasema la hasha! Abadan! Lazima CUF izuiliwe maana tuendako itakuwa hatari kubwa iwapo chama hicho kinachodaiwa kuwa adui wa Muungano kwa mtazamo wake wa mamlaka kamili, kitaachwa kama kilivyo.
Ndipo fursa ya tofauti katika mtazamo wa viongozi kwenye maoni ya Tume ya Jaji Joseph Warioba baina ya Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Shariff Hamad na pia kuundwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na hivyo pale Ukawa ilipojipanga kugombea kama jukwaa moja ikawa ndio fursa ya wazee wa ofisi mbalimbali kulikalia hilo.
CUF ikapasuliwa kwa Profesa Lipumba kudaiwa kutumika kwa kisingizio cha kutokubaliana na Ukawa ikiaminika alijiamini kuwa ni yeye ndio angeteuliwa kubeba bendera ya Ukawa dhidi ya John Pombe Magufuli na badala yake akateuliwa Edward Lowassa, ambapo kuna ushahidi kuwa ni yeye ndiye aliyempeleka ndani ya Ukawa.
Basi mengine ni historia. Mbaya sana. Ya CUF kupelekana mahakamani na kushuka mpaka Machi 19, 2019 historia ya siasa za Tanzania imefungua kitabu kipya kwa wanachama wa CUF kuhama kwa umoja wao, yaani wana na wazee kwenda ACT Wazalendo chama kipya katika rubaa za siasa chenye mrengo wa kijamaa kinachoongozwa na Zitto Kabwe.
Mtu anaweza kujiuliza swali hivi ni CUF iliyohamia ACT Wazalendo au ACT Wazalendo ndio imehamia CUF. Hayo ya mjadala huo yatakuja baadaye hasa kwa faida za kitaaluma, ila kwa sasa CUF wasiomkubali Profesa Lipumba ambaye naye jana alipewa uhalali wa kuwa Mwenyekiti na mahakama, wamemfuata Maalim Seif.
Naam Maalim Seif. Inaaminika ataondoka na maelfu ya wanachama wa CUF wasiomuafiki Lipumba huko Unguja na Pemba na hata huko Bara. Ni muhamo mkubwa kuonekana Tanzania, inawezekana Afrika Mashariki na pengine sehemu nyingine duniani. Ni hili pia siku za mbele inaweza kuwa hoja ya kitaaluma.
Maalim Seif amehama na watu kama Mpiga Filimbi wa Hamelin. Amewachukua watu wengi kwa mujibu wa picha zilizokuwa zikitembea mitandaoni juzi, kiasi ambacho kwa ghafla mtu anaweza kujiuliza hivi Profesa Lipumba atabakishiwa angalau ukoko huko Zanzibar? Sidhani. Na kwa kweli ni ngumu.
Si haki na si sahihi kuitambiria CUF ya Lipumba kifo, maana ni mapema na inawezekana ina mbinu kibindoni ya kukikuza na kukibakisha katika ramani chama hicho, ila itawawia vigumu sana, hasa ikiwa watategemea dola, badala ya kuja na mbinu za kisiasa kurai rai wananchi.
Wananchi wa Zanzibar waliokuwa CUF wakiongozwa na Maalim Seif wameyageuza mara moja matawi yote ya CUF kuwa ya ACT Wazalendo na hii ina maana CUF ya Lipumba inaanza upya kabisa na sijui kama hili lilikuwa katika mipango yao.
Inaanza pengine haina hata ofisi moja na kwa nijuavyo Wazanzibari itakuwa vigumu sana mtu kuwakodisha nyumba iwe ofisi, labda wasaidiwe na dola. Siamini pia watakodishwa nyumba kirahisi ili wafanye matawi Pemba. Huko sidhani hilo linaweza kutokea na itakuwa miujiza mikubwa likitokea.
Sasa yote haya yanatokea kwa sababu wanachama hao wa CUF walikuwa na imani kubwa na Maalim Seif na ndio hao waliokubali kuhama naye kwenda ACT-Wazalendo. Wamemjua Maalim Seif tangu akiwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar mwaka 1984 -1985, wamemjua tangu alipofukuzwa na Rais Idriss Abdul-Wakil pamoja na wenzake kadhaa kwa tofauti za ndani.
Wengi wanakumbuka Maalim Seif alivyokuwa mwanasiasa shupavu ndani ya CCM na kufika kushika Ujumbe wa Kamati Kuu na kuongoza Idara ya Uchumi ya chama hicho na Kamati Kuu wakiwemo akina Dk. Salmin Amour, Dk Salim Ahmed na Wazanzibari wengine kadhaa.
Wengi wanamkumbuka alipowahutubia katika Uwanja wa Tibirinzi, Pemba ambapo alisema atakuwa nao akiwa kwenye siasa na nje ya siasa, dhiki na raha. Amekuwa nao. Yupo nao kwa kila lililomfika na yaliyowafika wanachama wake. Hajawahi kuondoka. Na watu wake hawajawahi kuondoka, Wapo. Mpaka leo wapo naye.
Amefungwa, amenyan’ganywa haki za kustaafu, amenyanyaswa na sasa wamempoka hata chama ambacho yeye alikuwa ni sehemu ya waliokianzisha na amekuwa ni alama ya chama hicho na alama ya mapambano nchini Tanzania.
Kwa sasa hakuna. Kabisa. Mtu yeyote anayeweza kujidai kuwa na hadhi na haiba inayofanana na Maalim Seif. Mwenye sifa ya kuwa mwanasiasa mahiri, alama ya siasa za Tanzania kama Maalim Seif. Ni yeye ambaye amekuwa kivutio, tishio kwa siasa zozote za kistaarabu, ila amefanyiwa ubabe na vitisho vingi.
Kuhama kwake kutaleta mtikisikio wa kisiasa Tanzania na kutaleta sekeseke kubwa katika siasa za Tanzania Bara maana demokrasia kipindi hiki ilianza kuingiwa mtihani kwa kutiwa kitanzi. Hatua hii itakuwa chachu mpya.
Siasa ni nipe nikupe. ACT-Wazalendo wamempa nafasi Maalim na upande wake Maalim atawapa mengi ACT. Mengi mno kiasi ambacho wakiyatumia vizuri ni faida kubwa kwa nguvu ya Ukawa.
Kuelekea chaguzi zijazo mwaka huu na Uchaguzi Mkuu 2020 hali ya kisiasa ya Tanzania itachanua sana na iwapo hakutakuwapo na changamoto katika kujenga ushindani sawa na wa haki.
Hapana shaka Maalim, Zitto na CUF na ACT ni ushirikiano mzuri sana na kila chama kingependa kipate hali kama hiyo, ila hili si kama donda kila mtu hupata. Hii ni fursa adhimu, wapewao ni wachache.
Hii imekuwa kama hadithi ya Jahazi la Mtume Nuhu ambalo lilihama na kila kitu kutafuta salama na si tu salama yaani pia kuendeleza maisha na kwa hapa maisha ni kutafuta jukwaa jipya la siasa ambacho ndio kitu pekee Maalim Seif anachokijua.