Mwandishi wetu -Dodoma
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza kufanyika uhakiki wa kina katika utekelezaji agizo la wananchi kutoondolewa katika vijiji 920 vilivyokuwa na mgogoro na maeneo ya hifadhi nchini.
Kutokana na migogoro hiyo, Rais Dk. John Magufuli alitangaza kuvibakisha vijiji 920 kati ya 975 kwenye maeneo ya hifadhi yaliyokuwa na mgogoro.
Jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo kwa mawaziri wa wizara zinazohusika katika utekelezaji huo.
Wizara ambazo makatibu wakuu wake wanashiriki kazi ya utekelezaji wa agizo hilo ni Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Kilimo, Maji, Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akipokea ripoti hiyo kwa niaba ya mawaziri wengine, Lukuvi alisema katika kipindi hiki ambacho kamati za wataalamu zinapitia taarifa za utekelezaji wa maamuzi kuhusiana na suala hilo, lazima ufanyike uchambuzi wa kina.
‘’Ufanyike uchambuzi wa kina kuona faida itakayopatikana na vijiji vingapi vitanufaika na tupate taarifa itakayoainisha kila eneo na makubaliano yake,’’ alisema Lukuvi.
Alisema kila sekta inayohusika inatakiwa kufanya uchambuzi katika eneo lake, huku akitolea mfano Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo inaweza kuja na uchambuzi utakaoainisha maeneo ya EPZA.
Akiwasilisha ripoti yake, Makondo alisema kamati ya makatibu wakuu imeendelea kufanyia kazi utekelezaji maamuzi ya vijiji 920 kama walivyoelekezwa.
Alisema kamati hiyo katika kutekeleza maagizo ya mawaziri, inatarajia kukamilisha kazi ya tathmini ya vijiji 920 katika kipindi cha wiki mbili na kuwasilisha taarifa yake kwa mawaziri wa sekta.
Kwa muda mrefu wananchi wa vijiji 975 vilivyo katika hifadhi, wamekuwa katika mgogoro na hifadhi na baadhi makazi yao kuchomwa moto.
Mgogoro huo ulisababisha Rais Magufuli kuingilia kati na kuridhia vijiji 920 kubaki kwenye maeneo ya hifadhi sambamba na kufutwa misitu ya hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 ili ipangwe upya.
Pia Rais Magufuli alifuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa ekari 707,659.94 na ardhi hiyo kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya makazi, kilimo na shughuli za ufugaji.