Na AGATHA CHARLES, Dar es Salaam
CHADEMA na Chama cha ACT– Wazalendo, vimejibu tuhuma zilizotolewa na Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka.
Juzi Sendeka, alimtuhumu kwa kumshambulia Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kutokana na misimamo yao ya kukosoa mwenendo wa utawala wa Rais Dk. John Magufuli.
Kauli za kumjibu Sendeka zilitolewa kwa nyakati tofauti jana na vyama hivyo, vilipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi zao zilizopo Dar es Salaam.
Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT- Wazalendo, Habibu Mchange, akimjibu Sendeka, aliviomba vyombo vya uchunguzi nchini kuchunguza akaunti, mali na madeni ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini ili kupima kama yanaendana na maisha anayoishi.
Alisema wanavitaka vyombo hivyo kuanza mara moja kazi ya uchunguzi kwa kuwa wanaamini Zitto ni mmoja wa viongozi ambaye mali, madeni, masilahi na akaunti zake viko wazi.
“Ikumbukwe kuwa katiba na kanuni za chama chetu huwataka viongozi wote wa chama kuweka hadharani tamko la mali zao na madeni, Zitto alitekeleza matakwa hayo kisheria, mali pamoja na madeni yake yako hadharani na mtandaoni.
Tunatambua chama tawala kinaweweseka, tunataka kiondokane na ugonjwa huo, badala yake wachukue hatua za uchunguzi dhidi ya Zitto,” alisema Mchange.
Pia alimgeuzia kibao Sendeka kwa kumtaka kumkumbusha Rais Magufuli kuweka hadharani nyaraka zake za mshahara.
“Ole Sendeka amuulize mwenyekiti wake wa CCM ambaye ni Rais Magufuli kama bado yuko likizo. Alipokuwa Chato likizo, alipiga simu redio moja akasema akirudi ataweka ‘salary slips’ wazi, sasa bado yuko likizo? Tunapiga marufuku kumhusisha Zitto na siasa nyepesi,” alisema Mchange.
Akizungumzia kauli kwamba Zitto alikuwa akiwalinda maswahiba zake alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mchange alisema anashangazwa na kauli hiyo kwa kuwa Rais Magufuli amekuwa akipambana na ufisadi, lakini alishindwa kumchukulia hatua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau na badala yake akamteua kuwa balozi nchini Malaysia.
Mchange alisema katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kupitia taarifa husika alitoa hati safi kwa NSSF kwa hesabu za mwaka wa fedha wa 2014/2015 na hata katika barua ya mkaguzi kwenda kwa kiongozi wa NSSF, inaonyesha kuwa halijanunua ardhi yoyote Kigamboni bali liliingia ubia wa ardhi kwa hisa (Land for Equity).
“Sijui msemaji wa CCM anatumia taarifa ipi ya CAG kusema kuwa NSSF ilinunua ardhi kwa bei ya shilingi milioni 800 aliyomhusisha nayo kiongozi wetu. Sasa Mkurugenzi wa NSSF anayesema kapewa ubalozi, ukiangalia Mwenyekiti wa CCM anapambana na ufisadi, anamshindwa nini huyo? Ina maana anateua mafisadi kuwa balozi? Hivyo ni vizuri akieleza kwa undani ufisadi anaousema kwa kunukuu ripoti ya CAG kaitoa ukurasa namba ngapi,” alisema Mchange.
CHADEMA
Naye Mkuu wa Idara ya Uenezi wa Chadema, Hemed Ali, alimshambulia Sendeka akisema ni sawa na mtumishi hewa kwa kuwa cheo chake hakipo kikatiba kwa mujibu wa Katiba ya CCM na wala hakipo katika ngazi za utawala Makao Makuu ya chama hicho.
Hemed alisema hata taarifa aliyoitoa Sendeka ilikosa mtiririko wa kiuandishi na kimantiki, kuanzia utangulizi, ujumbe na hitimisho alivyodai havina uwiano.
Alisema hatua hiyo inatokana na kuwapa nafasi watu wasio na uwezo na kwamba hata kada mwenzake, Profesa Sospeter Muhongo, aliwahi kutahadharisha juu ya uongo wa Sendeka pamoja na kufeli masomo yake ya kidato cha sita kwa kupata daraja sifuri.
“Ole Sendeka anaendeleza mwendelezo wa Rais Dk. Magufuli wa kutokutaka kukosolewa na wataalamu, wanahabari na Watanzania kwa ujumla, wakisahau Katiba ya Jamhuri inawapa Watanzania uhuru wa kutoa maoni,” alisema Hemed.
Pia alisema hawashangai Sendeka kushambulia vyombo vya habari kwa kuwa CCM na Rais Magufuli hawapendi Watanzania watoe maoni, na ndio maana wanataka kusukuma Muswada wa Habari.
Akizungumza kuhusu mashambulizi aliyoyatoa dhidi ya Lowassa, Hemed alisema CCM inaugua homa yake inayoitwa Lowassaphobia.
“Ndiyo maana kimeacha kuendelea na shughuli zao na kumwandama Lowassa. Kimsingi mchakato wa kumpata mgombea urais na mgombea mwenza wa chama ulikuwa wa kidemokrasia kwa mujibu wa katiba yetu ambapo ibara (7.7.16 (a)), kamati kuu inapewa mamlaka ya kuwafanyia utafiti wagombea urais na kupeleka ripoti Baraza Kuu,” alisema Hemed.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ( 7.7. 13 (a)), Baraza Kuu linapendekeza majina ya wagombea au mgombea aliyejitokeza na kupitia Ibara ya (7.7.10 (c)), Mkutano Mkuu wa chama unachagua mgombea urais na mgombea mwenza.
Alisema Lowassa alipitia hatua zote kama mwanachama halali wa Chadema kwa mujibu wa Katiba (5.1) na (5.2).
Pia alikumbushia mchakato wa kumpata mgombea wa urais kupitia CCM mwaka 2015 kwa kuuita kuwa haukufuata katiba na kanuni za chama hicho.
“Nilitarajia Sendeka aeleze kile kiini macho cha kumchagua Magufuli Dodoma kuwa mgombea wao, huku wenyewe kwa wenyewe wakipinga mchakato wa kumpata usiofuata katiba na kanuni za chama hicho kama walivyojitenga na uamuzi huo baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa uamuzi ndani ya vikao. Kamati Kuu yao ilipasuka katikati baina ya wajumbe,” alisema Hemed.
Alisema anakubaliana na Sendeka kuwa mgombea ni taswira ya chama, lakini alidai kuwa CCM kwa sasa inaonyesha ni wafinyaji na wakandamizaji wa demokrasia.
Akijibu tuhuma za kiongozi mmoja wa chama kupatiwa Dola milioni 15 za Marekani takriban Sh bilioni 33 za kitanzania, alisema fedha hizo ni nyingi na zingetosha kuchukua madaraka kamili kuanzia ngazi ya mtaa hadi urais na si tu kupanga safu ya ndani ya chama.
“Amesema kuwa yupo kiongozi ndani ya chama chetu aliyepata dola milioni 15 apange safu ya uongozi ndani ya chama. Kiuhalisia na kwa hesabu ndogo tu ni kuwa pesa hiyo si tu inatosha kupanga uongozi wa ndani, bali ushindi wa mitaa, kata na halmashauri, ubunge na urais, hivyo wakati anataja tarakimu hizo ajue na michanganuo ya hesabu badala ya kuwa mkurupukaji,” alisema Hemed.