25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 18, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU: MAUMIVU NI MAKALI SANA

NA WAANDISHI WETU –DAR/DODOMA

LICHA ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kuelezwa kuwa inaendelea kuimarika, jana  alikaririwa akisema maumivu anayoyasikia ni makubwa ambayo hajawahi kuyapata.

Hayo yalielezwa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa, Ezekiah Wenje, ambaye yupo Nairobi kumjulia hali  Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu.

Akieleza hali ya Lissu ambaye jana amemaliza wiki moja akiwa kwenye chumba maalumu cha uangalizi (ICU), baada ya kufanyiwa upasuaji mara tatu Wenje aliema. “Tumetoka hospitalini tayari. Lissu is doing well (anaendelea vizuri).

“Ana maumivu makali sana. Leo amesema hajawahi kusikia maumivu kama leo (jana). Anaongea vizuri na Mungu wetu atamponya ,”alisema Wenje.

Juzi Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji aliwaambia waandishi wa habari kuwa Lissu alivunjwa mguu wa kulia zaidi ya mara tano, mguu wa kushoto, nyonga na mkono wa kushoto.

Mnyukano wa Ndugai, wabunge

Wakati hali ya Lissu ikiendelea hivyo, mvutano wa Spika Job Ndugai na wabunge wake umeendelea ambapo baada ya kumalizana na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), upepo sasa umehamia kwa wabunge wa Chadema na mvutano ukiwa ni nani alilipia ndege iliyompeleka Lissu Nairobi.

Ndugai na wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Peter Msigwa (Iringa Mjini), wameingia kwenye mvutano huo mpya, ambapo jana Spika  alizungumzia video ya Lema iliyorushwa mtandaoni juzi ambayo pamoja na mambo mengine, mbunge huyo alilaumu Bunge kutoshughulikia matibabu ya Lissu na badala yake kuchangisha wabunge posho zao, akisema Ndugai mwenyewe alitibiwa na fedha nyingi tu za Serikali.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai alizungumzia video hiyo huku akimshangaa Lema na kusema hata fedha za kukodi ndege iliyompeleka Lissu Nairobi, zilitolewa na  Mbunge wa CCM ambaye ni Salim Hassan Turky wa Jimbo la Mpendae.

Kauli hiyo ya Ndugai ilimuibua Mchungaji Msigwa ambaye alirekodi video kama alivyofanya Lema juzi, akimtaka Spika kuacha uongo kwani ndege hiyo imelipiwa na Chadema.

Naye Turky, alisema  hakulipa fedha za ndege hiyo bali alichofanya ni kuwadhamini Chadema ili ndege hiyo imsafirishe Lissu kwa sababu yeye ana uhusiano wa karibu na kampuni inayomiliki ndege hiyo na kwamba, Chadema walilipa fedha za ndege hiyo jana mchana.

Ndugai na Lema

Jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai alilieleza Bunge jinsi alivyosikitishwa  na kauli za Lema, huku akisema yeye Spika, serikali na wabunge wa vyama vyote walihangaika kuanzia mchana mpaka usiku wa manane na Lema anayetoa shutma sasa hakuwepo.

Alisema hata fedha za kukodi ndege kiasi cha dola za Marekani 9200 (Sh milioni 20.634), zilitolewa na Turky ambaye ni mbunge wa CCM.

Ndugai alisema. “Waheshimiwa wabunge kwa mnaofuatilia vyombo vya habari, mmemwona mheshimiwa Lema akinishambulia mimi na leo nitajitahidi kuongea kwa upole sana sana.

“Lema amenishutumu ni kwanini nimeagiza mheshimiwa Kubenea akahojiwe na kamati za Bunge. Wakati anayasema hayo, mheshimiwa Lema hayupo hapa bungeni na kwa maana nyingine, hajui kinachoendelea ingawa nyinyi wabunge ndiyo mlioamua hapa mambo ya ulinzi na usalama yaende kwenye kamati baada ya mheshimiwa Bashe kuwasilisha hoja hapa.

“Katika maelezo yake, Lema anasema kutokana na mheshimiwa Lissu kushambuliwa, Bunge lingesimamisha shughuli zake, wakati anajua kanuni zetu zinasema ili Bunge lisimamishe  shughuli zake ni pale mbunge mwenzetu anapofariki. Sasa anataka Bunge lisimamishe shughuli kwa sababu zipi?

“Lakini, kwetu sisi tunaomfahamu Lema, hatuwezi kumshangaa, kwa leo namsamehe kwa sababu hajui alitendalo.

“Lema anasema Serikali imegoma kugharimia matibabu ya Lissu wakati suala hili nililieleza siku ile hapa bungeni kutokana na majadiliano tuliyoyafikia kati ya Serikali, familia ya Lissu pamoja na mheshimiwa Mbowe.

“Siku ile nilisema baada ya Lissu kushambuliwa, gari iliyotumika kumpeleka hospitalini, ni ya familia ya Naibu Spika ambaye ni mbunge wa CCM na hata madaktari waliomtibu pale hospitalini ni madaktari wa Watanzania na hao hao ndiyo waliosababisha apate nafuu na kusafirishwa kwenda Nairobi.

“Nilisema pia kwamba, pale hospitalini, viongozi wa Serikali walikuwapo, alikuwapo Waziri wa Afya, alikuwapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alikuwapo Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, alikuwapo mheshimiwa Msigwa, alikuwapo Silinde, nilikuwapo mimi, alikuwapo Mbowe na walikuwapo wabunge wengi wa Chadema, CCM na CUF.

“Yeye Lema hakuwapo, lakini sasa yuko Nairobi anaanza kunishutumu mimi, hivi hii ni sawa, au huu ndiyo upinzani?

“Hata wakati mgonjwa anasafirishwa kwenda Nairobi, wabunge na Serikali tulishirikiana kumsafirisha mwenzetu, lakini Lema hakuwapo na leo yuko Nairobi anaanza kunishutumu, hii siyo sawa kabisa.

“Wakati Lissu yuko hospitalini, Serikali ilikuwa imeshaleta ndege yake hapa ikisubiri ahamishiwe Muhimbili kwa matibabu zaidi, sasa tujiulize ni mgonjwa gani aliwahi kusubiriwa na ndege kama Lissu miongoni mwa wabunge wetu.

“Nilisema siku ile, kwamba wabunge wote tuna bima za afya za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambazo zinaturuhusu kutibiwa katika hospitali zote za umma na inaposhindikana, rufaa yetu ni Muhimbili na ikishindikana, rufaa yetu ni Hospitali ya Apolo, India ambako mimi na viongozi mbalimbali tumetibiwa huko kwa nyakati tofauti.

“Kwa taarifa yenu, baada ya Mbowe kusema wanataka kumpeleka mgonjwa Nairobi, mbunge wa CCM, Turky (Salim Hassan Turky, Jimbo la Mpendae), alikubali kukodi ndege kwa Dola za Marekani 9,200 ambayo ndiyo ilimpeleka mgonjwa Nairobi baada ya Serikali na sisi kuitafutia vibali vyote vilivyokuwa vikitakiwa kuruka kutoka hapa Dodoma kwenda Nairobi.

“Hivi kweli aliyoyasema Lema ndiyo gharama za Spika, hivi kweli nyinyi ni watu wa Mungu, yaani nimeruhusu Bunge tumchangie Lissu Sh milioni 43, halafu leo mnanishambulia.

“Anasema eti shambulizi la Lissu lilikuwa ‘organized’, lakini hili ni la ulinzi na usalama naamua kuliacha ila nawaambia wananchi wa Arusha kwamba Arusha ‘deserves better’, alisema Spika Ndugai.

“Kutokana na maelezo hayo, Lema kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika. “Mh Spika nashukuru kwa msamaha wako wa bure, lakini mimi na familia yangu tumechagua kuendelea kukuombea,” alisema.

Turky azungumzia uhusika wake

Nje ya viwanja vya Bunge, Turky alisema. “Tusifanye tukio la Tundu Lissu tukataka kufanya siasa, tukio la Lissu limenisononesha sana na nikiwa kama kamishna wa Bunge lakini zaidi ni binadam ambaye ninaamini kuna kuzaliwa na kufa, tukio hilo lilipotokea tuliitwa na Spika.

“Makamishna tukakaa na bahati nzuri alikuwepo Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), Msigwa na mimi, Spika na timu yake madaktari na Waziri wa Afya  (Ummy Mwalimu), sote tukashirikiana pale, yaliyopita yamepita lakini kuhusu ndege, kwanza ndege ilikuwepo, ambayo ilikuwa imeagizwa na Bunge.

“Ilikuwa iko tayari kumpeleka mgonjwa Muhimbili, kilichotokea wenyewe (Chadema) wakaamua mgonjwa aende Nairobi, ndege ile ilikuwa haina vibali vya kwenda Nairobi, ili uende Nairobi inabidi wawe marubani wawili, Spika aliangaika mpaka akaipatia kibali ile ndege ili iende Nairobi, wakati mambo yote yakwa tayari rubani wa ndege akasema kuna kitu kinaitwa Landing instrument, ambayo ile ndege ilikuwa haina ili iweze kuta Nairobi.

“Hapo tukawa njia panda, mimi nikatumia uwezo niliojaliwa na Mungu nikatafuta ndege kwa flight link ambao ni ndugu zetu tunafanya nao biashara sana.

“Nikawaambia kwamba ndege ipo wakatoa nauli zao za ghalighali, lakini kwasababu tunajuana wakakubali kutusaidia kwa dola 9,200 pamoja na ambulance.

“Kwa hiyo ile ndege mimi ndiye niliyeiita, kwa kukubaliana na mwenyekiti wa Chadema bwana Mbowe na bwana Msigwa kwamba Turky haya mambo yasimamie, sisi tutakuja kuyaweka sawa na ndicho kilichotokea.

“Kwa hiyo wao walivyofika kule ilikuwa siku ya pili warekebishe mambo lakini hawakuweza, Jumatatu imepita, Jumanne, Jumatano jana imepita naona leo Bungeni watu wameanza kuzungumza, na nafikiri katika taarifa ya Spika alizungumza kwamba bwana Turky ametoa fedha hizo  na Chadema watalipa.

“Ni kauli ambayo haina matatizo kwasababu kama Chadema wasingelipa mpaka leo, ilikuwa nitoe fedha zangu nilipe kwasababu wale mabwana watakuwa wameshapitiliza fedha zao, lakini bahati nzuri mchana wa leo saa 6:30 (mchana) nimempigia mwenye ndege ndiyo Chadema wameenda kumlipa.

Swali: kwa maana hiyo wewe uliingia udhamini wa mali kauli tu?

Jibu: Ndiyo lakini mali kauli hiyo yako haikubaliki yangu inakubalika kwasababu anajua hapa zipo, walikuwa wanataka kauli ambayo ina hakika kama upande wa pili haujalipa huyu bwana anayetudhamini atalipa.

Swali: Kwa hiyo hukutoa fedha taslimu?

Jibu: Hapana siyo cash na bahati mbaya au nzuri siku ile ile ndege isingeweza kuruka kama zisingepatikana dola 9,000, kwa maana lazima hela ulipe ndiyo ndege iruke na hapa Dodoma hakuna aliyekuwa na dola hata 1,000 kwa hiyo ilikuwa kidogo hali ngumu lakini nashukuru Mungu penye nia njema hufungua milango yake.

Swali: Au una hisa kwenye hizi ndege?

Jibu: Hapa hizi ndege sihusiki na lolote, ni rafiki yangu ambaye naruka naye sana na wagonjwa wengi tunapokuwa tunao basi mara nyingi wanajua huyu bwana ana connection, hizi ndege ni za ETG, (Export treading  group) ndiyo ndege yao.

Msigwa

Baada ya kauli ya Ndugai, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, aliweka katika mitandao ya kijamii, nyaraka zinazoonyesha Chadema ndiyo waliolipia ndege hiyo baada ya kuchangishana na wala si Turky kama Spika alivyoeleza.

Mbali na nyakara hizo, video ya Msigwa pia ilisambazwa kwenye mitandao ambapo pamoja na mambo mengine alisema. “Nakuheshimu sana Spika kama kamishana wa Bunge lakini mwenendo unaokwenda nao namna unavyoliongoza Bunge na jinsi Serikali ilivyoteka, imekumeza unashindwa kuliongoza Bunge, ni lazima kuyasema haya japo najua consequence (matokeo) ya haya.

“Leo (jana) asubuhi umelipotosha Bunge kwa kusema uongo kwamba ndege iliyokodiwa imelipwa na mbunge wa CCM…naomba Ndugai umwogope Mungu, Chadema ndio imelipa gharama za ndege.

“Nakuchukulia kuwa wewe ni adui wa usalama wa taifa la Tanzania, kwa sababu unasabaisha mhimili wa Bunge uwe dhaifu kwa sababu Serikali imekuteka inakupa maagizo na unafanya Bunge liwe butu lishindwe kusimamia maamuzi na kuisimamia Serikali.

“Nasema haya kwa ujasiri mkubwa kwa sababu kitu gani cha kuogopa tena kama ndugu yetu ameshapigwa risasi na tumeshaambiwa anayefuata sasa ni Mbowe, Lema, mimi na Halima (Mbunge wa Kawe, Halima Mdee) tuko kwenye list ya kupigwa risasi.

“Tuogope kusema nini ikiwa Bunge umelifanya kuwa butu tukilalamika Bunge liseme ni kwa sababu ya ubutu wa kutokusimamia Serikali kama inavyopaswa.

“Nataka niseme kwa sababu hakuna cha kuogopa tutasema mpaka mwisho kwa sababu uhai wetu na usalama wa nchi yetu umetishiwa kiwango cha juu sana lakini Ndugai wewe kama Spika una sifa gani kutuambia tuwe na adabu ndani ya Bunge.

“Huna moral authority (mamlaka) ya kutuambia tuwe na adabu ndani ya Bunge wakati wewe wakati wa kampeni ulipiga mtu kwa fimbo ulitakiwa uwe gerezani si kusimamia nidhamu ndani ya Bunge tunashindwa wakati mwingine kuwaambia watoto wetu kuwa wewe ni kiongozi wa Bunge.

“Unaposhindwa na kututisha bungeni na kutufukuza bungeni kutupiga pingu alright … Mimi nasimama tena mbele yako na mbele ya umma na dunia nzima niko tayari kufukuzwa bungeni lakini hatutanyamaza kwa sababu umeshindwa kulisimamia Bunge,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles