Ramadhani Hassan -Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu, mapato ya ndani yaliyokusanywa ni Sh trilioni 11.87, sawa na asilimia 92.3 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 12.86.
Alisema mapato hayo ni sehemu ya Sh trilioni 33.11, za bajeti ya 2019/20 ikijumuisha Sh trilioni 20.86 matumizi ya kawaida na Sh trilioni 12.25 kwa matumizi ya maendeleo.
Dk. Mpango alisema kati ya makusanyo yaliyofikiwa hadi sasa, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh trilioni 10.62 sawa na asilimia 96.9 ya makadirio ya Sh trilioni 10.96.
Alisema kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa kukusanya mapato ya kodi umeimarika na kufikia asilimia 96.9 ya lengo ikilinganishwa na asilimia 88.6 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019.
“Sababu za ongezeko la mapato yaliyokusanywa na TRA ni pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya walipakodi, wananchi kuhamasika kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu wezeshi ya barabara na umeme.
“Sababu nyingine ni kuendelea kuongezeka kwa uwazi katika usimamizi wa sheria za kodi, maboresho ya huduma kwa mlipakodi, usimamizi wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki, hususan kwenye sekta ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, kuendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kuwashirikisha kikamilifu na kuwaelimisha ipasavyo wale wote ambao wamekuwa wakibainika kukwepa kodi,” alisema Dk. Mpango.
Alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato ya kodi, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza makusanyo zaidi.
Alizitaja hatua hizo ni pamoja na kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kodi, kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti unatumika ipasavyo.
“Kuendelea na utoaji wa elimu kwa mlipakodi na dhana ya ‘Ukinunua Dai Risiti na Ukiuza Toa Risiti’; kuendelea kuongeza kasi katika utatuzi wa pingamizi za kodi, kuendelea kusimamia matumizi ya stempu za kodi za kielektroniki (ETS) katika bidhaa,” alisema Dk. Mpango.
WAHISANI, SERIKALI ZA MITAA NA WIZARA
Dk. Mpango alisema mapato yasiyo ya kodi yaliyokusanywa na wizara, idara zinazojitegemea, taasisi na wakala wa Serikali yalikuwa ni Sh bilioni 835.3.
Alisema Mamlaka za Serikali za Mitaa zilikusanya Sh bilioni 412.6, sawa na asilimia 90.2 ya makadirio ya Sh bilioni 457.4 kwa kipindi hicho.
Dk. Mpango alisema katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, washirika wa maendeleo walitoa Sh trilioni 1.58, sawa na asilimia 95.2 ya makadirio ya Sh trilioni 1.66.
Alisema kiasi hicho kimeongezeka kwa asilimia 46.6 ikilinganishwa na kilichopokewa Julai 2018 hadi Januari 2019.
MIKOPO
Dk. Mpango alisema hadi Januari 2020, Serikali imefanikiwa kukopa Sh trilioni 3.04 kutoka soko la ndani sawa na asilimia 100.9 ya lengo la Sh trilioni 3.01.
Alisema kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 2.23 zilitumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na Sh bilioni 806.8 zilitumika kugharamia miradi ya maendeleo.
Dk. Mpango alisema mwenendo wa upatikanaji wa fedha kutoka soko la ndani umeimarika kutokana na kuongezeka kwa ukwasi kwenye benki za kibiashara na Serikali kuendelea kutoa matangazo ya minada ya dhamana za Serikali katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
“Hadi Januari 2020, kiasi cha Sh trilioni 1.82 sawa na dola za Marekani milioni 800 kimepatikana kutoka Benki ya Biashara na Maendeleo (Trade and Development Bank – TDB). Kiasi hicho ni asilimia 98.3 ya lengo la kukopa Sh trilioni 1.85 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
“Aidha, kiasi kilichobaki cha dola za Marekani milioni 200 kinatarajiwa kupatikana kutoka benki hiyo,” alisema Dk. Mpango.
MATUMIZI
Dk. Mpango alisema kwa upande wa matumizi kwa mwaka 2019/20, Serikali ilipanga kutumia Sh trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.
Alisema kati ya Julai 2019 hadi Januari 2020, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya Sh trilioni 18.27 ikijumuisha fedha za washirika wa maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Serikali imetumia Sh trilioni 5.80 kulipia deni la Serikali lililotokana na mikopo iliyotumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo,” alisema Dk. Mpango.
VIPAUMBELE
Dk. Mpango alisema katika mwaka 2020/21, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuongezeka na hivyo kuweza kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati.
“Vipaumbele vitakuwa katika kuendelea kuboresha mazingira ya uendeshaji biashara na uwekezaji kwa kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini ili kukuza biashara ndogo na za kati kwa ukuaji endelevu wa uchumi.
“Pia kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari pamoja na upanuzi wa wigo wa kodi na kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato.
“Vilevile kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya Tehama.
“Pia kuwianisha na kupunguza tozo na ada mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji na kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania.
“Vilevile kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu na mikopo inayotolewa kwa utaratibu wa udhamini kutoka taasisi za udhamini wa mikopo,” alisema Dk. Mpango.
Alisema Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria ya bajeti sura 439, Sheria ya Fedha za Umma sura 348 na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa.
“Lengo kuu ni kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na miradi mingine muhimu.
“Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la uzalishaji wa madeni ya Serikali,” alisema Dk. Mpango.