27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kurejereza taka ni utajiri uliojificha nchini

bsf

Na Joseph Lino,

Kampuni ya kurejereza taka ya Recycler Tanzania, inatarajia kuanza uzalishaji wa funza kwa kutumia mabaki ya taka ya vyakula na mimea.

Funza hao wana protini kwa wingi  kuliko dagaa hutumika kama chakula cha mifugo ikiwemo kuku, nguruwe, samaki na viumbe vingine.

Kutokana na wingi wa taka ngumu za vyakula mkoani Dar es Salaam, Kampuni ya Recycler Tanzania imeanzisha mradi wa kuzalisha funza kupitia teknolijia ya kisasa utakaosaidia kupunguza taka ngumu ya vyakula katika baadhi ya maeneo.

Meneja wa miradi wa Recycler, Phillipo Stephen anasema  mradi huu ambao unaelekea katika hatua za mwisho utaanza  kuzalisha funza kwa kiwango kikubwa kuanzia Januari mwakani.

“Funza hawa  wana virutubisho vya protini kwa asilimia 40 na ambayo ni zaidi ya iliyoko kwenye dagaa, funza wanatumika kama chakula cha mifugo kama kuku, nguruwe na samaki,” anasema.

Mradi huu ambao utakuwa wa kwanza nchini utazalisha funza takribani tani moja kwa siku, na itasaidia kupunguza kiwango cha taka ya mabaki ya chakula na mimea kwa maelezo ya Recycler.

Mchakato wa uzalishaji funza unaanzia kwa inzi maalumu ambayo wanafungwa na kulisha taka ngumu ya vyakula kabla kuwa funza.

‘Funza wa aina hii wanatokana na mayai ya inzi, ambayo yanawekwa katika vifaa maalumu na kabla kufikia hatua ya  kuwa inzi tunawachukua,”.

Anasema katika hatua hiyo huwa wanaanikwa na kuwekwa katika vifungashio.

Kampuni hiyo kwa sasa inazalisha kwa kiwango kidogo kwa ajili ya majaribio ambapo wanasubiri vifaa kutoka Marekani.

“Tunatarajia kuanza uzalishaji mkubwa wa zaidi ya tani moja kwa siku, na funza watauzwa kwa gharama dogo ukilinganisha na  bei ya dagaa,” anasema.

Katika kuelezea miradi mingine ya kampuni, anasema kuna mradi wa kuzalisha nishati ya umeme kutumia taka ngumu.

“Mradi huu unatumia taka ngumu ambazo haziwezi kuchakatwa kuzalisha umeme, aina ya taka hizo kama mifuko ya rangi nyeusi ya sandarusi  ambapo  hii haiwezi kuchakatwa na badala yake inaweza kutengeneza nishati ya umeme,” alisema.

Stephen anaongeza kuwa  kuna taka ngumu nyingi katika maeneo mengi yanaoyozunguka jijini kama Buruguruni, Mwananyamala na maeneo mengi taka nyingi zinaenda kutupwa.

Mradi wa kuzalisha umeme upo katika majaribio ya awali na hivi karibuni utakuwa katika majaribio.

Aidha, alifafanua namna sekta ya uchakataji au kuhuisha taka  na kuitaja kuwa  ni biashara yenye utajiri uliyojificha ambayo bado watu hawana uelewa wakutosha namna wanaweza kunufaika.

“Dhana ya uchakataji taka ni kutengeneza bidhaa mpya kutoka bidhaa ya zamani ambayo imeshatumika tumika na kutupa kama taka,” anasema Stephen.

Sekta ya uchakataji taka Tanzania bado ipo nyuma ambapo asilimia nyingi ya taka huishia kutupwa bila kujua thamani  ya taka badala ya utengenezaji bidhaa mpya.

Mkoa wa Dar es Salaam huzalisha taka kiasi cha tani 3,000 kwa siku na chini ya asilimia 40 au tani 120 tu hutumika katika uchakataji kwa mujibu wa Recycler.

Na kiasi ambacho kinaenda katika uchakataji ni kidogo kulinganisha na taka zinazopatikana  sehemu mbalimbali za jiji.

Stephen anasema mlundikano wa taka maeneo mengi limekuwa tatizo kubwa  na sugu ambalo linahitaji ufanisi wa hali ya juu kulitatua.

“Biashara ya uchakataji taka Tanzania bado haijajulikana  kutokana watu kukosa  uelewa wa kutosha kuhusiana na sekta  na rasilimali hii,”.

Recycler inaamini sekta hii inaweza kubadili maisha ya watu wengi kama itapewa kipaumbele kwa kutoa ajira, kuokoa mazingira yanayoharibika kutokana na taka hizi ambazo zinalundikana bila kufanyiwa kazi.

Kampuni inajihusisha na taka rejereza na kutunza mazingira, kampuni ya Dar es Salaam Recycler ilianza shughuli zake rasmi mwaka 2014.

Ni moja ya kampuni zinazotarajia kuleta mabadiliko katika sekta ya uchakataji taka ikiwa na baadhi ya miradi yake.

Kwa upande wa hali ya biashara hii nchini, Stephen anaelezea kuwa makampuni mengi ya uchakataji yamejikita katika plastiki zilizotumika, lakini kuna taka za aina nyingi ambazo zinazalishwa.

Sekta hii ina wadau wengi ambao ni serikali, makampuni binafsi, wananchi, watu wanaozalisha taka.

Biashara hii inashindwa kufanikishwa  vizuri, kutokana kukosekana kwa sera na miongozo ya Serikali ya kusimamia sekta hii.

“Kama kungekuwapo na sera ambayo mzalishaji taka awe anawajibika kuchakata kwa kila anachozalisha, hali hiyo inaweza kuboresha sekta ya uchakataji na kuwa tegemeo kwa wananchi,” anasema Stephen.

Anaelezea kwamba iwapo serikali ingemwajibisha wanaokiuka uchakataji wa taka hizo, wanaozalisha taka angekuwa na nidhamu, na hivyo kuweka nidhamu ya uhifadhi mazingira.

 

Hata hivyo, sekta hii inahitaji uwekezaji mkubwa na makampuni mengi yaliyopo nchini bado ni machanga kiufanisi, miondombinu na teknolojia inayotumika pia ni duni.

“Kutokana na uelewa mdogo kuhusu suala hilo miongoni mwa jamii, serikali inahitaji kuweka mkono wake, hasa katika makampuni makubwa ili waelekeze nguvu katika  kudhibiti na kuwajibika katika uchakataji taka,”

Kwa maelezo ya kampuni ya Recycler, taka zinazotupwa zinagharimu kiasi kikubwa cha pesa, ambapo mzalishaji anaweza kuokoa kiasi cha shilingi  200 kwa kilo moja ya plastiki ikiwa plastiki ngumu unaokoa shilingi 500, kwa mifuko ya sandarusi ataokoa shilingi 300.

Kampuni ya Recycler inafanya uchakataji wa aina nyingi za taka kwa pamoja, kwa mwezi huchakata  wastani  wa tani 100,  na tani 150 kwenda kutupwa jalalani.

Kampuni inategemea kufanya kazi na wadau mbalimbali wakiwemo viwanda, shule, mabalozi, na baadhi ya wenye nyumba.

Kampuni hiyo huchakata karatasi nyeupe, maboksi, glass, magazeti, mbao, chuma, vifaa vya eletroniki, kama friji, simu na taka zingine.

Katika ripoti ya benki ya dunia kuhusu maendeleo ya miji, inaonesha kuwa Afrika huzalisha tani milioni 70 kwa mwaka.  Ripoti hiyo inasema kuwa ongezeko la idadi ya watu wanaohamia mijini inaongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa taka kufikia tani milioni 160 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

“Uwepo taka ambazo hazikusanywi ni tatizo ambalo linasababisha uchafuzi wa mazingira, magonjwa na majanga ya mazingiria,” ripoti inasema.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles