28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

KURA YA CCM YAIPA USHINDI UKAWA

Na CHRISTINA GAULUHANGA – DAR ES SALAAM


DIWANI mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amempigia kura mgombea wa kiti cha Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mussa Kafana aliyekuwa akigombea kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kutokana na kura hiyo ya diwani wa CCM ambaye hakujulikana, Kafana (Diwani wa Kiwalani kupitia CUF), alishinda kwa kura 12 dhidi ya kura kumi alizopata mgombea wa CCM, Mariam Lulida.

Wakati wa uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, wajumbe waliokuwa wakitokana na Ukawa walikuwa 11 na CCM pia 11.

Awali, uchaguzi huo ulikuwa ufanyike jana asubuhi, lakini hadi saa sita mchana ulikuwa haujafanyika kwa sababu mgombea Kafana alikuwa hajafika ukumbini kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa amelazwa katika hospitali ambayo haikutajwa jina na mahali ilipo.

 

UKAWA WAGOMA

Taarifa za ugonjwa wa Kafana ambaye alitakiwa kutetea nafasi yake, ziliwashtua wajumbe wa Ukawa na kuweka msimamo wa kutoendelea na uchaguzi hadi atakapopatikana ingawa simu zake za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.

Akizungumzia kuhusu taarifa hizo za ugonjwa, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita (Chadema), aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo wa uchaguzi, aliwaambia wajumbe kwamba alipigiwa simu na mwanamke mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mke wa Kafana, akimweleza kuwa mgombea huyo ametundikiwa drip hospitalini.

Kutokana na hali hiyo, Meya Mwita, aliungana na wajumbe wengine wa Ukawa kugoma kushiriki uchaguzi huo.

 

ATEULIWA MWENYEKITI MWINGINE

Wakati wapinzani hao wakifikia uamuzi wa kugoma, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana, aliamuru ateuliwe mwenyekiti mwingine ili aendeshe kikao hicho cha uchaguzi.

Spora alisema pamoja na kuwapo kwa dalili za uchaguzi huo kutofanyika kama ulivyopangwa, wajumbe wanatakiwa kuelewa kwamba umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara na kwamba jana asingekuwa tayari kuuahirisha.

Baada ya vuta ni kuvute kati ya wajumbe wa CCM na Ukawa, wajumbe wa CCM walimteua Meya wa Temeke , Abdallah Chaurembo, akakae meza kuu kuendesha kikao hicho.

 

UKAWA WACHACHAMAA

Wajumbe wa Ukawa walipomwona Chaurembo akiwa kwenye meza kuu, walichachamaa na kupinga utaratibu huo, huku wakimwondoa kwa nguvu.

Miongoni mwa wajumbe waliokwenda kumtoa kwenye meza kuu Chaurembo, ni Diwani wa Segerea, Patrick Assenga na Meya wa Ubungo, Boniphace Jacob wote wa Chadema.

Tukio hilo lilisababisha vurugu za hapa na pale na kudumu kwa zaidi ya nusu saa.

 

WATAKA UCHAGUZI UAHIRISHWE

Kwa upande wake, Meya Jacob alimtaka Meya wa Jiji (Mwita) kutumia utu kwa kuwa mgombea Kafana ambaye amefanya naye kazi zaidi ya mwaka mmoja, hapatikani na simu yake haipokewi.

“Naona Mwita umejisahau na hutaki kutumia utu, kama mtu ambaye umefanya naye kazi zaidi ya mwaka hapatikani na simu yake haipokelewi, wewe unaonekana kutojali, hili ni jambo la kusikitisha.

“Wajumbe wa CCM wanaonekana hawajali kwa kuwa wameahirisha uchaguzi huo mara nyingi kwa sababu zisizo na tija, lakini suala la ugonjwa la mgombea wa Ukawa wanalipuuzia,” alisema Jacob.

 

MKURUGENZI AAMURU UCHAGUZI UENDELEE

Pamoja na maelezo hayo, Spora alisema amechoshwa na vurugu zinazolinyima Jiji la Dar es Salaam maendeleo na kuamuru uchaguzi huo uendelee huku akiteuliwa Jacob kumwakilisha Kafana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles