Derick Milton, Bariadi.
Mgombea ubunge jimbo la Bariadi Andrea Kundo (CCM) amewaomba wananchi wa vijiji vya Itubukilo, Mwanzoya na Halahala kata ya Itubukilo kumpigia kuraili iwe mwisho wa kero ya kutokuwa na umeme pamoja na Barabara zinazopitika.
Kundo ametoa ahadi hizo mbele ya umati wa wananchi wa vijiji hivyo leo katika mwendelezo wa kampeini zake, ambapo aliwaeleza wananchi hao kama wanataka kutatuliwa kero hizo basi wamchague awe mbunge wao.
Amesema kuwa amejionea kero ya barabara inavyowatesa wananchi hao hasa barabara kuu ambayo inaingia na kutoka ndani ya vijiji hivyo, kutoka katika kata ya Ngulyati, Mwanzoya hadi kata ya Sakwe.
“ Wakati ninakuja nimepitia barabara hii, lakini kabla ya kampeini kuanza nilikuja hapa nikaambiwa kero hii, wananchi wengi wanalia nah ii barabara, ni kweli hali ni mbaya, hamna barabara, mnateseka sana.
“ Nataka niwaleleze hapa, endapo Oktoba 28, mtakwenda kufanya kama vile nawaomba, mkinichagua mimi, Diwani wa CCM pamoja na Rais Magufuli, ndiyo utakuwa mwisho wa kero hii,” amesema Kundo.
Hata hivyo Mgombea huyo amehaidi neema kwa vijana wa jimbo hilo, ambapo ataunga mkono shughuli zao za michezo kwa kutoa vifaa vyote vya michezo katika kila kata, huku akihaidi kuanzisha mashindano ya kata kwa kata, hadi jimbo.
“ Lengo langu ni kuhimairisha Afya za vijana, katika kutimiza hilo, nitahakikisha natoa vifaa vya michezo kila kata, na kuanzisha mashindano ya kata hadi jimbo, na hili nitalisimamia mimi mwenyewe maana nitakuwa na uwezo nalo,” amesema Kundo.
Aidha Mgombea huyo alihaidi kutatua kero za madereva pikipiki (Bodaboda), ambazo ni kukamatwa kila wakati katika kujitafutia ridhiki, kuwa atahakikisha anatumia nafasi yake ya ubunge kusimama nao wakati wote.