24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kumbilamoto atekeleza ahadi Kipunguni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary kumbilamoto, amekabidhi televisheni na feni kwa vijana wanaojifunza ushonaji katika Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni.

Mwanzoni mwa mwaka huu Kumbilamoto alitembelea shirika hilo na kuguswa namna ambavyo linawalea vijana na kuahidi kuwapa vifaa hivyo.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto (katikati), akikabidhi feni kwa vijana wanaojifunza ushonaji katika Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni. Kulia ni Mkurugenzi wa shirika hilo, Seleman Bishagazi.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Kumbilamoto amelipongeza shirika hilo na kutoa wito kwa vijana walioko mtaani kujitokeza kwenda kupatiwa mafunzo.

“Nawapongeza sana Sauti ya Jamii kwa kazi nzuri mnayofanya, nilipokuja hapa niliona vijana wanajifunza kushona lakini kuna mazingira ya joto nikasema nitawaletea feni na ‘tv’ ili wanapokuwa wanaendelea na shughuli zao wawe wanaburudika kwa kuangalia tv lakini pia wasikumbane na adha ya joto,” amesema Kumbilamoto.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Sidde, amelipongeza shirika hilo na kusema shughuli wanazozifanya ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo pia inahimiza kuwawezesha vijana kushiriki katika ujasiriamali.

Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kutangaza utekelezaji wa ilani ambao umefanyika kwenye maeneo yao.

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaendelea kutekelezwa kila kona, hata haya yanayofanyika hapa (Sauti ya Jamii Kipunguni) ni utekelezaji la Ilani, kuna mambo mengi mazuri yanafanyika, tokeni nje mkayaseme ili watu wayajue,” amesema Sidde.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Kipunguni, Gamaliel Mhanga, amesema shirika hilo limekuwa likisaidia makundi ya vijana na kinamama kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali, usaidizi wa kisheria na kupambana na vitendo vya ukatili.

Mlezi wa shirika hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba, amesema “Shirika hili limekuwa msaada mkubwa katika mtaa wangu hasa kaya masikini zinazohudumiwa na TASAF zimenufaika sana.

Viongozi hao pia wamekagua ofisi mpya ya shirika hilo ambapo Kumbilamoto ameahidi kutoa vifaa vya jipsum na mikanda yake ili kumalizia ujenzi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, ofisi hiyo wanayojenga kwa fedha zao wenyewe imegharimu zaidi ya Sh milioni 11 ambazo zinajumuisha pia ununuzi wa eneo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles