Na LEONARD MANG’OHA
SERIKALI kupitia Waziri wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na Mazingira, January Makamba, imekuwa ikipiga kelele kuhusu uchafuzi wa mazingira hususan unaotokana na taka za plastiki.
Sehemu nyingine ni fukwe za bahari, mitaro ya kuondolea maji taka katika miji mbalimbali mikubwa kwa midogo na maeneo yote ya makazi yamefurika taka za aina hii, jambo linalofanya taka hizo kuonekana kama vile ni sehemu ya maisha ya wakazi wa miji karibu yote.
Mfano taarifa zinaonesha kuwa mifuko ya plastiki inaweza kuelea majini hadi miaka 400 bila kuharibika, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi kutokana na ukweli kwamba, inahatarisha uwapo wa viumbe wa majini ikiwamo samaki.
Matumizi ya vifungashio vya plastiki yanaongezeka kwa kasi ya ajabu tena bila  kudhibitiwa na watumiaji, hakuna anayejali kuhusu usalama wa maisha ya viumbe hai wa majini dhidi ya madhara ya mifuko hiyo.
Inaelezwa kuwa ifikapo mwaka 2050 uzito wa taka za plastiki majini utazidi uzito wa samaki baharini, jambo ambalo ni hatari kwani hakutakuwa na malisho ya uhakika kwa viumbe wa majini kutokana na taka hizo kuchukua nafasi yake.
Picha halisi inayojijenga hapa ni kwamba, hadi mwaka huo badala ya wavuvi kuvua samaki wataanza kuvua plastiki hivyo kuathiri uchumi wao na dunia kwa ujumla.
Kuendelea kutapakaa kwa taka hizi kutapunguza malisho ya mifugo kutokana na hatari yake, hususan mifuko ya plastiki ambayo hukatisha haraka maisha ya wanyama pale inapotokea wamekula mifuko hiyo ambayo huziba utumbo na kuoza na kuwasababishia kifo.
Kabla madhara haya hayajaongezeka na kuwa makubwa kiasi cha kutishia maisha ya dunia na viumbe wake, jamii ya kimataifa inapaswa kufanya uamuzi mgumu wa kuzuia matumizi ya vifungashio vya plastiki katika shughuli za kila siku ili kupunguza hatari ya kimazingira inayoinyemelea dunia.
Kama jamii ya kimataifa ilivyoweza kudhibiti kampuni zinazotengeneza bidhaa za tumbaku kujitangaza kupitia vyombo vya habari na kudhamini michezo mbalimbali, vivyo hivyo wanapaswa kutoa msimamo katika matumizi ya plastiki isitumike kabisa na kuzuia utengenezwaji wake.
Kukemea pekee kuhusu uchafuzi wa mazingira si suluhisho la kumaliza tatizo hili, kwani limeendelea kukua licha ya kutolewa matamko ya kiserikali mara kadhaa.
Naamini jamii ya kimataifa inayo nguvu ya kumaliza hili, kwani inao uwezo wa kuzitaka nchi wanachama kutunga sheria itakayowabana watengenezaji wa vifungashio badala ya kutengeneza plastiki watengeneze vifungashio vinavyoweza kuoza kwa muda mfupi baada ya kutumika.