Na Christian Bwaya,
TUMETAJA mambo mawili yanayobadili mfumo wa malezi. Mosi, ni kubadilika kwa majukumu ya kijinsia yaliyozoeleka katika jamii. Mama anapoingia kwenye soko la ajira na kwenda kazini kama ilivyozoeleka kwa baba changamoto inayojitokeza ni namna wanavyoweza kumlea mtoto wao katika muda wa kazi.
Pili ni kufifia kwa utamaduni wa familia tandao unaozorotesha msaada wa kimalezi uliozoeleka kutoka kwa ndugu wa karibu. Mawili haya yanalazimisha familia za sasa kutafuta namna nyingine ya malezi kuwapa fursa wazazi kuendelea na kazi.
Katika makala haya tunatazama huduma ya akina dada wanaoajiriwa kuwasaidia wazazi kulea watoto wakati wa kazi, maarufu kama ‘house girls’.
Namna ‘house girls’ wanavyopatikana
Hawa ni watoto au vijana wadogo waliokulia katika mazingira ya kawaida, mara nyingi kijijini tena bila elimu kubwa, wanaoajiriwa na wazazi kwa lengo la kuwasaidia kumtazama mtoto wakati wa kazi. Sambamba na malezi, wasichana hawa hufanya kazi za ndani.
Kwa kawaida walezi hawa hupatikana kwa utaratibu usio rasmi unaotegemea mfumo wa kufahamiana na ndugu, jamaa na marafiki wanaoweza kuwaunganisha wazazi wenye uhitaji na msichana anayetafuta kazi. Hakuna utaratibu rasmi unaowawezesha waajiri wenye uhitaji kuwa na uhakika na historia yake, ujuzi wake pamoja na tabia zake kwa ujumla.
Hata hivyo, hutokea wakati mwingine wakapatikana kupitia kwa watu wanaofahamika. Ingawa utaratibu huu wengine huuchukulia kama namna nyingine ya usafirishaji wa binadamu, lakini umekuwa ukiwasaidia wazazi kuwa na uhakika na wapi hasa watoto hawa wanatoka.
Mazingira yao ya kazi
Mara nyingi mabinti hawa huajiriwa bila mikataba inayoeleweka na hulipwa kiasi kidogo cha fedha. Hata hivyo, nje na malipo ya fedha taslimu, wazazi wengi huwapa marupurupu kama chakula, matibabu na huduma zingine za msingi.
Ratiba zao za siku hujaa shughuli nyingi zisizolingana na kipato chao. Wengi wao huwa wa kwanza kuamka na wa mwisho kulala. Waajiri wao huwa na matumaini makubwa kupindukia.
Pamoja na kazi kubwa wanazofanya, yamekuwepo matukio ya wasichana hawa kuonewa na waajiri wao kwa namna mbalimbali. Wapo wanaotendewa kama watumwa wasiostahili heshima kama binadamu wengine. Wengine hunyimwa haki zao za msingi.
Katika mazingira haya, wasichana hawa wakati mwingine hujenga tabia zisizofaa ambazo huzorotesha uhusiano wao na waajiri wao. Hali ya kutokuelewana kati ya mwajiri na mtoto huyu wa kazi husababisha hasira, uchungu na visasi ambavyo mara nyingi huishia kwa mtoto asiye na hatia.
Utendaji wao kimalezi
Kwa kawaida wasichana hawa ambao mara nyingi ni watoto, huwa hawana uzoefu na malezi. Utendaji wa wengi wao hutegemea maelekezo ya kila mara. Hata hivyo, pamoja na hayo bado wazazi wenye uwezo mdogo kiuchumi huwaona kama jawabu la changamoto ya malezi.
Kwa upande mwingine yamekuwapo matukio ya akina dada hawa kuwafundisha watoto tabia zisizofaa kwa kujua au kutokujua. Haya, hata hivyo, mara nyingi hufanyika kulipiza kisasi kwa hisia za kutokutendewa haki.
Kwa ujumla, pamoja na faida ya kuwatumia akina dada hawa zinaripotiwa changamoto nyingi ambazo zina uwezekano wa kuwaathiri watoto moja kwa moja. Katika makala ijayo tutatoa mapendekezo ya namna tunavyoweza kuboresha huduma inayotolewa na akina dada hawa wa malezi.
Itaendelea.
Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815