HATUWEZI  kushindana nao kwenye uwanja ambao wao wameweka miundombinu yao na vyombo ambavyo vinawatumikia. Ukija kama mgeni ni vigumu kusoma mazingira kabla hujapata funguo za kusoma na kuelewa yalipo.
Ni kama kuingia kwenye nyumba ngeni, hauwezi kuingia kama huna funguo na ukishaingia utumiaji na uangaliaji wa hiyo sehemu ni wajibu wako. Tofauti zinaweza kuwa ni kubwa kwenye utumiaji na uangaliaji wa hiyo sehemu. Uangalizi unabebwa na miaka mingi ya malezi ambayo umepata.
Wengine wanaishi tu bila ya kufahamu kwamba usipoziba ufa utajenga ukuta. Wengine wanaweza kuingia ndani ya nyumba hata kama ni mbovu, kutokuona kunatokana na sababu mbalimbali pia ambazo ni za kibinafsi.
Ufa unatokana na mambo mengi mojawapo ni kwa sababu msingi unaweza kuwa haukukaa vizuri, au uwiano kati ya simenti na mchanga haikukaa sawa, au saizi ya matofali si sawa.
Ukifika sehemu ambayo ni ngeni kwako ni rahisi kufanya kama wenyeji kuliko kuzingatia yale ya hekima unayoyajua na uliyokulia nayo. Kufuata yale ambayo hujapata ufunguo wa kukuwezesha kuelewa, mara nyingi yatakukwamisha na kuleta uhasama kati ya nafsi yako na mazingira mapya. Kutokufahamu kunaweza kukuchanganya.
Kama ni mtu ambaye unaelewa na umekulia katika mazingira ambayo yamekupa funguo kukuwezesha kuuliza na kutafuta habari ya jinsi ya kuishi katika mazingira mageni basi mpito na uwezo wa kukabiliana na hali hiyo mpya unakuwa ni rahisi. Unaingia katika uwanja au nyumba na nyenzo ambazo zitakusaidia kuelekeza.
Kwenye kujenga nyumba unaanza kwanza kusafisha eneo. Muhimu kufahamu jinsi nyumba itakavyokaa haswa kama unataka kupata upepo mzuri kutoka baharini au sehemu nyingine kama za baridi sana jinsi utavyovuna jua, au makaro ya uchafu yamekaa sehemu ambayo yanastahili ili harufu usipate au huenda sehemu za kupumzika au jikoni.
Wakati wote huu una ramani ambayo inakuongoza kwenye ujenzi, ambao ni mfumo wa kiutendaji, hapa ni watu wamekaa na kupanga jinsi nyumba itajengwa mpaka ifike hapo wanaweza kuhamia. Uwiano ya sementi, unaangalia kama msingi unaweza kubeba uzito wa kiasi ambao umetathiminiwa.
Unaangalia uimara wa tofali na kama hizi tofali zinafaa kujenga ghorofa? Nondo Milimita ngapi na usuka ngapi utatandikwa chini na zinakwenda kwenye nguzo mpangilio, kokoto unaangalia.
Wakati tunajenga jumuiya yetu iwe Ughaibuni au ndani ya nchi yetu Tanzania, misingi mizuri ni muhimu sana. Kwani bila misingi mizuri matatizo mengi yataibuka. Tunahitaji kuimarisha msingi unaobeba uzito wote wa jumuiya hasa zile nguzo zinazoshikilia ujenzi unaoendelea juu ya huo msingi.
Bila hivyo hakuna mabadiliko yoyote yatakayoonekana na uimara utapotea jinsi unavyojenga juu. Udhaifu unaoendelea hapo chini utaangusha nyumba siku moja na jitihada zote nzuri ambazo zimewekwa zitapotea.
Matakwa ya jamii ni muhimu yazingatiwe na pia kufahamu ni jinsi gani jamii itasimama kwenye mazingira yaliyopo au kama ni nyumba basi ardhi ya pale, kuifahamu ni ya namna gani kabla hujasimamisha nyumba.
Uzito wa jengo au jamii lazima ikae kwenye misingi imara. Kufahamu ni udongo wa aina gani itatuwezesha kufahamu ni malighafi gani zitatumika kujenga jumuiya. Zingine hazifai kwani sio sehemu ya utamaduni wetu.
Wakati ujenzi wa jumuiya yetu unaendelea Ughaibuni changamoto ni nyingi na haswa kuelewa kwamba uwanja na mazingira ambayo tupo ni tofauti sana na ya kwetu na hapa ni kufahamu huu sio uwanja wetu. Tunajenga jumuiya juu ya ardhi ya watu wengine ambayo mizizi yao imeenda chini sana. Lakini msingi yao ipo na tunaweza kujitahidi kutumia hiyo msingi kama tukitafuta na kupata huo ufunguo na kuutumia ipasavyo. Ujenzi ukiendela kwenye msingi imara utaona kwamba nyumba yako itasimama imara na kuweza kupambana na changamoto zozote zile ambazo zitatupwa kutoka pande zozote. Ni muhimu dira, dhima, malengo na madhumuni yaeleweke na mfumo wa kiutendaji uwepo.
Nilipanda bodaboda jijini Dar s Salaam kwenda kwenye mkutano ambao nilikuwa nimeshachelewa, katika mazungumzo yangu na mjasiriamali akanielezea matatizo ya bodaboda wanayoyapata, mojawapo ni jinsi wanavyonyanyaswa mitaani na watu ambao wamewekwa kulinda na kusaidia jamii. Wanapigwa faini kubwa sana kila wakati. Kila sababu zinatafutwa kwa wao kuwekwa chini ya ulinzi. Ni mfumo gani ambao upo hapo kuwanyanyasa hawa wajasiriamali ambao kipato chao ni kidogo sana, Je, kuna wengine ambao wapo katika mazingira kama haya? Huu ni mfumo ambao unatoka wapi? Wapi ambapo jamii imekosea na kuruhusu hali kama hii? Huu ni ufa mkubwa katika jamii yetu. Na ufa za aina hii zipo nyingi katika jamii yetu, hata huduma ambazo unastahili kupewa kutoka kwenye taasisi tofauti.
Ughaibuni ni tofauti kutokana na kwamba mazingira ambayo yapo haya matatizo hayapo. Wao wameweza kupalilia na kuondoa miundombinu ambayo inawaumiza wajasirimali wadogo wadogo.