*Ndugai azuia wabunge watakaoziweka wasiingie bungeni
* Wanaharakati wadai amedhalilishwa utu wa mwanamke
Na WAANDISHI WETU-DAR/DODOMA
Hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kupiga marufuku wabunge waliobandika kucha na kope bandia kutoingia ndani ya ukumbi wa Bunge, imeibua mjadala huku wanaharakati wakidai kiongozi huyo amedhalilisha utu wa mwanamke.
Spika Ndugai alitoa marufuku hiyo bungeni jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu, baada ya Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Tawfiq (CCM), kuhoji idadi ya wanawake walioathirika macho kutokana na matumizi ya kope bandia.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Dk. Vicencia Shule, alisema kauli ya kiongozi huyo wa Bunge, imelenga kudhalilisha wanawake.
Alisema watanzania wana shida nyingi za msingi ambazo zinapaswa kujadiliwa bungeni lakini si kuingilia uhuru binafsi wa mtu kwa mujibu wa Katiba.
“Kwanza hilo alilolisema lingekuwa lina umuhimu ingewekwa kwenye kanuni na sheria za kibunge, lakini isiwe tu utashi wa mtu na pia kama wameamua kuangalia hayo pia iwe pamoja na nywele bandia kwa sababu mle bungeni asilimia kubwa wana nywele bandia.
“Lakini kama imeamuliwa iwekwe kwenye kanuni, lakini si utashi wake vinginevyo akiamka kesho atasema leo hakuna kujipuliza perfume au hakuna kupaka wanja, kimsingi ameingilia uhuru binafsi wa mtu.
“Kauli yake inalenga udhalilishaji kwa wanawake…watanzania wana shida za msingi kama maji, afya, elimu ambazo zinatakiwa kujadiliwa bungeni lakini si kauli kama hizi ambazo hazina manufaa kwao.
“Pia kwa kauli yake ameweka mtego anajua mbunge yeyote akijitokeza kupinga kesho atamwita akahojiwe kwenye kamati kuwa analidhalilisha Bunge wakati yeye ndiye anayedhalilisha.
“Atuambie pia ni utaratibu au vigezo gani vitatumika kukagua hao wabunge kuwa wana kope au kucha bandia watashikwa au,”alihoji Dk. Shule.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alisema kauli hiyo ya Ndugai ni ukiukwaji wa haki za wanawake na ni ukatili wa kijinsia.
“Tunailaani kauli ya Ndugai, ni kauli inayotweza utu wa wanawake. Nawashauri Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG) walivalie njuga suala hili,”alisema Henga.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema), alisema Spika atakuwa alitania kwa sababu hakuna kanuni zinazozuia watu wasibandike kope au kucha.
Alisema kanuni zilizopo ni za mavazi pekee kanuni zambazo zinazuia kuvaa nguo fupi au iliyobana sana maungo, kofia au nguo zenye mwelekeo wa itikadi fulani ya chama.
“Haiwezekani kuwazuia wabunge wasifanye hivyo, utazuiaje wakati ni uhuru binafsi, kuongeza makalio, kujichubua ni uamuzi wa mtu binafsi haiwezekani kuzuia,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Sonia Magogo (CUF), alisema haiwezekani zuio hilo likafanya kazi na kuhoji ukaguzi huo utakavyofanyika.
“Spika ana utani sana atakuwa alitania tu kwa sababu atajuaje huyu amebandika kope au kucha, au ukaguzi huo utafanyika vipi, kwanza halipo wala halihusiani na kanuni za kudumu za Bunge,” alisema Sonia.
AGIZO LA NDUGAI
Jana, baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Fatma Tawfiq (CCM), Spika Ndugai alisema anapiga marufuku wabunge kuingia bungeni wakiwa na kope za kubandika na kucha.
“Kutokana na elimu hiyo na mimi leo napiga marufuku kwa wabunge wote kuingia bungeni wakiwa na kucha na kope bandia, lakini kwa wale wanaojichubua naendelea kuchukua maoni,” alisema Spika Ndugai.
Mara baada ya kusema hivyo baadhi ya wabunge wanaume walipaza sauti kwa kusema kuwa na wa nywele bandia nao wasiruhusiwe kuingia.
Aidha, akijibu swali la mbunge huyo, Dk. Ndungulile alisema kwa sasa wizara kupitia Mamlaka Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) haina utaratibu wa kudhibiti kope wala kucha za kubandika kwa sababu hakuna sheria inayoipa ya kudhibiti bidhaa hizo.
“Hivyo basi, kutokana na hilo wizara kupitia TFDA, haina takwimu za kuonesha madhara yaliyotokana na bidhaa hizo kwa kuwa hakuna mfumo wa kupokea taarifa za matumizi ya bidhaa husika,” alisema
Pia Dk. Ndungulile alisema anaomba kuwapa somo wabunge huhusiana na kujichubua ngozi.
“Tunapojichubua ngozi zetu tunaondoa kinga, mtu anayejichubua ngozi anaingia katika hatari ya kupata saratani, magonjwa ya ngozi, rangi ya asili ni nzuri ilitengenezwa kwa ajili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hivyo nawaomba msiharibu ngozi zenu kwa vipodozi,” alisema