SEOUL, KOREA KUSINI
RAIS wa Korea Kusini, Moon Jae-in amesema atasaidia kufanikisha mkutano wa tatu wa kilele baina ya Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na Rais Donald Trump wa Marekani.
Moon amesema kabla ya mkutano huo, yuko tayari pia na kwa mkutano wa nne baina yake na Kim ili kusaidia kuokoa majadiliano yanayolega ega ya kinyuklia kati ya Washington na Pyongyang.
Matamshi ya Moon jana yanakuja baada ya Kim mwishoni mwa wiki kuikosoa vikali Korea Kusini, akiita mpatanishi aliyekiuka majukumu yake.
Kim ameitaka nchi hii jirani kujiondoa kutoka Marekani na kuunga mkono msimamo wa Korea Kaskazini zaidi.
Moon alikutana na Kim mara tatu mwaka jana na pia kuwa mpatanishi wa mazungumzo ya kinyuklia kati ya Marekani na Korea kaskazini kufuatia hali ya wasi wasi iliyojitokeza kutokana na majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini na vitisho vya vita kati ya Kim na Rais Trump.