Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limemtangaza Ammy Conrad Ninje kuwa kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, itakayoshiriki mashindano ya Chalenji, yatakayoanza Desemba 3 hadi 17, mwaka huu, nchini Kenya.
Ninje, ambaye ni raia wa Tanzania, amekuwa na mafanikio kwa vijana katika Academy ya Hull City ya Uingereza na anatarajia leo kutangaza majina ya wachezaji watakaounda kikosi hicho kitakachoshiriki mashindano hayo wakianza kuvaana na Libya Desemba 3, katika mchezo wa ufunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutambulishwa Dar es Salaam jana, Ninje alisema kuwa, anatarajia kutangaza kikosi chake leo, baada ya kumaliza kupitia kwa mara ya mwisho majina ya wachezaji atakaosafiri nao kwenda Kenya.
“Nimefundisha soka nchini Uingereza kwa miaka 14, lakini hapa nchini nimefundisha kwa miezi mitatu, naamini tutafanya vizuri na kurejea nyumbani na kombe,” alisema Ninje.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema kocha huyo amepewa timu hiyo kutokana na uzoefu wake katika soka la kimataifa, lakini pia uwezo wake mzuri wa kufanya kazi.