Na RAYMOND MINJA, IRINGA
ELIMU ndio ufunguo wa maisha. Hivyo, ili mtoto awe na maisha mazuri ni sharti kumpatia elimu na malezi mema. Hii itamsaidia kumjengea msingi bora wa maisha yake ya hapo baadae.
Mtoto ana haki ya kupata elimu nzuri kuanzia ngazi ya awali hadi elimu ya juu, hii itamsaidia kufanya vema katika masomo yake bila ya kupata vikwazo.
Awali wanafunzi wa shule za msingi walikuwa wanamaliza darasa la saba bila ya kujua kusoma na kuandika, hii ilisababishwa na wanafunzi hao kutokuandaliwa tangu wakiwa wadogo.
Kutokana na changamoto hiyo, Serakali iliamua kutafuta mwarobaini wa jambo hilo, na kuamua kuja na mbinu mbadala ya (KKK) Kuhesabu, Kusoma na Kundika, ambayo imeeanza kuleta mafaniko chanya katika mikoa mbalimbali ikiwamo Iringa.
USAID Tusome Pamoja ni mradi wa elimu wa miaka mitano unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID).
Mradi huu unalenga kusaidia kuboresha stadi za ufundishaji na KKK katika shule za awali na madarasa ya chini ya shule za msingi (1-4), katika mikoa minne ya Tanzania Bara (Iringa, Morogoro, Mtwara na Ruvuma) pamoja na shule zote za serikali visiwani Zanzibar.
Pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu, vitabu kwa wanafunzi, malengo zaidi ya mradi wa USAID Tusome Pamoja ni kuimarisha ushiriki wa wazazi na jamii kwenye elimu kupitia kamati za shule, Ushirikiano wa Wazazi na Walimu (UWAWA) na jamii yote kwa ujumla.
Hivi majuzi, USAID Tusome Pamoja ikishirikiana na Serikali mkoani Iringa iliendesha mafunzo ya Mpango Jamii wa Uhamasishaji na Utekelezaji Elimu (MJUUE) wenye lengo la kuhamasisha jamii kubaini changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu na zinazo athiri ubora wa elimu na ufaulu.
Mafunzo haya yalilenga (kusaidia jamii ishiriki katika kuandaa mipango ya elimu kwa ajili ya watoto wao hivyo kuimarisha ushiriki wa jamii katika kuboresha utoaji wa elimu kwani suala la maaendeleo ya shule linapaswa kufanywa na jamii husika na si serekali pekee.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wawili kutoka shule za msingi wilayani Kilolo, mkoni Iringa juu ya umuhimu wa jamii kushiriki shunguli za maendeleo ya shule, Ofisa Mradi wa Tusome Pamoja ndugu Wiston Ngowo anasema jamii inapaswa kutambua kuwa wana wajibu wa kuasidia maendeleo ya shule.
Ngowo anasema pamoja na kuwa mradi wa tusome pamoja ni kuhakikisha wanafunzi wanajua KKK lakini pia unawejengea uwezo wazazi kujenga utamaduni wa kushiriki shughuli mabalimbali za maendeleo ya shule zinazowazunguka na kuachana na dhana potofu ya kuwa shule zinapaswa kuhudumiwa na Serekali pekee.
Ngowo anasema suala la elimu ni la jamii nzima na si Serekali pekee, mabadiliko makubwa ya elimu yataletwa na wananchi wa sehemu husika na wala hayawezi kushuka kama baraka kutoka mbinguni.
Anasema mradi wa Tusome Pamoja uliobuniwa na Serekali na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID) umesaidia kwa kiasi kikubwa kubadili mawazo hasi waliyokuwa nayo wanananchi juu ya kushiriki shunguli mbalimbali za maendeleo shuleni ikiwamo kujenga majengo na vyoo bora.
“Hapo awali, wazazi wengi walikuwa ni wagumu kushiriki shunguli za maendeleo shuleni na walidhani kila kitu kinatakiwa kufanywa na serekali lakini baada ya mafunzo tuliyoyatoa, wamaebadilika na matokeo chanya yamenza kuonekana,” anasema.
Ngowo anasema mradi huo umefanikiwa kutoa elimu kwa walimu na maafisa elimu ikiwamo kutoa mafunzo ya KKK ili kumsaidia mtoto wa darasa la kwanza na la pili.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Keneth Komba anasema sasa hivi wazazi na walezi wanashiriki vema shunguli za kimaendeleo katika shule zinazowazunguka na wanafunzi sasa wanafanya vema katika KKK.
Anasema mradi huu umezifikia shule za msingi 481 zilizopo Iringa na baadhi wa walimu wanakiri uelewa umeongezeka kutokana na walimu kupewa mafunzo ya kisasa ili kuwa na mbinu mbadala ya kufundishia na kuacha kufundisha kwa mazoea.