25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KKK; TATIZO LINALOWAKOSESHA AMANI WANAFUNZI NANYAMBA

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanyamba, Msafiri Mtanda

Na FLORENCE SANAWA, NANYAMBA

MKOA wa Mtwara ni moja kati ya mikoa inayotajwa kuwa nyuma kielimu, licha ya juhudi nyingi zinazofanywa na serikali ili kuweza kuiondoa hali hiyo inayoathiri wanafunzi wengi, huku baadhi yao wakimaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

Katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, tatizo hili linaibainika katika Shule ya Msingi Nanyamba, hali inayowatesa  baadhi ya wanafunzi wasiojua kusoma shuleni hapo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanyamba, Msafiri Mtanda anasema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya watoto kushindwa kusoma na kuandika, hali inayowapa wakati mgumu walimu.

Anasema baada ya kutambua kuna baadhi ya wanafunzi uelewa wao ni mdogo, walimu walijipanga na kuweka mikakati ya kuwafundisha kwa muda wa ziada ili watambue KKK – Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Mikakati hiyo iliwezesha wanafunzi kupata muda wa zaida wa kujifunza KKK hali iliyowafanya waendelee kuwapo kwenye madarasa yao huku wakitumia muda wa ziada kuwapa mbinu mbalimbali za kuwawezesha kujua KKK.

“Hali ya kitaaluma kwa kiasi Fulani inaridhisha, hata ufaulu ni mzuri, hatujashuka chini ya asilimia 98, ndio maana tulipobaini uwapo wa wanafunzi wasiofahamu KKK katika shule yetu, ilitulazimu kuongeza nguvu.

“Asilimia 20 ya wanafunzi hapa shuleni hawajui kusoma lakini wanaonyesha moyo wa kujifunza, ndio maana walimu wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kuwa wanafanikiwa.

“Kwa kawaida watoto wasiojua kusoma huwa wanaathirika kisaikolojia, utakuta darasani kuna wanafunzi wawili hadi watatu ndio hawajui KKK hali hiyo huwaweka katika mazingira magumu. Wakati mwingine huchekwa na kutaniwa, ndio maana tumekuwa tukiwarudisha madarasa hata mwaka huu wapo ambao hawakuweza kufanya mtihani wa darasa la saba, wamerudia ili wajifunze zaidi,” anasema Mtanda.

Anasema kuwa watoto ambao ni watoro darasani ndio wanaoongoza kwa kutokujua KKK, wakifuatiwa na wale watukutu.

“Pamoja na hilo, wanafunzi wanalundikana mno darasani, mfano darasa la nne kuna wanafunzi 104. Jambo hili linachangia watoto kutokujua KKK kwa kuwa inamuwia vigumu mwalimu kuweza kumfikia kila mwanafunzi kwa wakati, hili nalo ni tatizo linalotukabili ndio maana mwaka huu tumepunguza idadi ya wanafunzi wa kujiunga darasa la kwanza,” anasema na kuongeza kuwa:

“Pia shule haina vitabu vya kutosha vya haiba na uraia. Pia uhaba wa nyumba za walimu unawafanya waishi mbali na shule.”

Naye Josephine Libaba, Mkazi wa Mtimbwilimbwi Halmashauri ya Mji Nanyamba ambaye ni mhamasishaji elimu, anasema miundombinu mibovu ya shule nayo inachangia kuzorotesha ubora wa elimu kwa walimu na wanafunzi huwa katika mazingira yasiyo rafiki.

“Wazazi hawana utaratibu wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni, wanawaachia suala hili walimu pekee, ndio maana watoto wengi wanafeli.

“Ushirikiano wa Wazazi na Walimu Shuleni (Uwawa), ukiwa endelevu utasaidia kuboresha elimu. Unajua kuna wakati ulifika baadhi ya watoto walikuwa wanafika darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, hii ilikuwa haitujengi na ilikuwa ikiongeza idadi ya wajinga vijijini lakini mradi huu  wa tusome pamoja utalifanya tatizo hilo liwe historia,” anasema.

Kwa upande wake Swahele Mpota, mkazi wa Kijiji cha Mnivata Halmashauri ya Mji Nanyamba anasema uwapo wa mradi huo umesaidia jamii kuelewa wajibu wao katika kufanikisha maendeleo ya watoto wao shuleni badala ya kuwaachia walimu pekee.

“Unajua katika suala la elimu hasa ya msingi, jamii iliwaacha walimu wahangaike wenyewe ndio maana hata makazi yao na miundombinu ya kufundishia haikuwa rafiki na wala haikuwa na muda hata wa kufuatilia masomo darasani, lakini kupitia mradi huu utasaidia kutatua changamoto za kielemu zinazotukabili kwa kiasi kikubwa,” anasema Mpota.

Mmoja wa wanafunzi ambao hawajui kusoma Razak Saidi (13) anasema kutokujua kusoma na kuandika hakuna tofati na mtu mwenye ulemavu.

Anasema kitendo hicho kilikuwa kikimuumiza kichwa kutokana na wanafunzi wengi darasani kumtenga na hivyo kuamua kuwa mtoro shuleni.

Mtoto huyo anasema mahudhurio yake hafifu yalimfanya  mwalimu mkuu wa shule hiyo awakusanye wanafunzi wote wasiojua kusoma na kuanzisha darasa maalumu ili kuwakazania zaidi katika masomo.

“Awali nilikuwa sijui kusoma kabisa, nilikuwa kama mtoto hadi wanafunzi wenzangu walikuwa wakinitenga, sikuwa na furaha hata walimu walivyokuwa wakinirudisha darasa nilikuwa naumia na kujihisi vibaya. Sasa hivi najitahidi kuhakikisha kuwa nasonga mbele,” anasema Said.

Naye mtoto Abdulahman Hamis (15) anasema tatizo la kutokujua kusoma kwa upande wake lilichangiwa na wazazi ambao walimuacha muda mwingi acheze badala ya kumsihi asome.

Anasema hali hiyo ilimfanya achukie shule na kuhusudu zaidi michezo.

“Zamani nilikuwa napenda sana kucheza badala ya kusoma, hata muda wa muda wa kula nilikuwa sina, shule ndio nilikuwa siipendi kabisa sikutaka hata kuonekana.

“Kwa sababu hiyo, KKK kwangu ilikuwa ni shida, wazazi wangu nao hawakujali, lakini nawashukuru walimu walinikazania hadi leo hii najua KKK,” anasema Hamis.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles