Na HASSAN DAUDI
KUTOKA utumizi wa barua, kisha sanduku la posta, na sasa utumizi wa simu na barua pepe, hakika maendeleo ya sayansi na teknolojia yamekuwa na mchango mkubwa kwenye nyanja ya mawasiliano.
Hata hivyo, licha ya utitiri wa kompyuta, bado simu imeonekana kuwa ‘silaha’ yenye ushawishi mkubwa katika kupashana habari. Huenda zipo sababu nyingi za simu kuendelea kuwa kimbilio la wengi, lakini kubwa ni urahisi wa kuitumia, achilia mbali unafuu wake ukilinganisha na kompyuta.
Kuthibitisha kasi ya matumizi ya simu ilivyo kubwa, watumiaji wa simu nchini walifikia milioni 43, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Hata hivyo, hakuna namna ya kulipa kisogo kundi la vijana unapozungumzia ushawishi wa simu katika jamii. Ni rahisi tu kusema hao ni sehemu kubwa na muhimu unapogusia nguvu ya kifaa hicho cha mawasiliano.
Nikiongeza katika hilo, hata umiliki wa simu wa vijana nao umekuwa na upekee wake ukilinganisha na ule wa wazee wao. Mathalan, haishangazi kuona simu ya babu au bibi ina mfumo mwepesi wa uendeshaji, tofauti na aliyonayo kijana wake mwenye umri wa miaka 20.
Kwa kijana, aghalabu itakuwa simu ya kisasa (smart phone), wakati kwa babu yake ‘simu ya tochi’ inafaa kwa matumizi ikiwa tu haitakuwa na changamoto ya kumfanya ashindwe kuwasiliana na aliyempigia.
Wakati babu akihitaji simu ya mawasiliano pekee, kijana wake ameenda mbali zaidi na kutamani yenye kamera nzuri, uwezo wa ‘kutembea’ kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia vifurushi, au ukubwa wa utunzaji kumbukumbu.
Sasa, tofauti ya makundi hayo hauiishii katika umiliki wa aina za simu, bali pia hata namna ya kupashana habari. Hapo ndipo ninapoliona tatizo kwa vijana na kushawishika kuandika makala haya.
Kwa utafiti wa kawaida tu, unaweza kubaini kuwa mtindo wa kutumiana meseji (kuchati) katika kundi hili umetawaliwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa lugha yao adhimu ya Kiswahili.
Kati ya meseji 10 wanazoweza kutumiana vijana, zaidi ya nusu yake ni Kiswahili cha ajabu aidha, kwa maneno yasiyo sanifu, muundo mbovu wa sentensi, au matumizi yasiyo sahihi ya alama za uandishi, achilia mbali mseto wa Kiswahili na Kiingereza, wengine wakiuita kwa jina la Kiswanglishi.
Vifupisho kama ‘vp’ (vipi), ‘asnt’ (asante), ‘lkn’ (lakini), ‘ktk’ (katika), ‘p’ (poa), ‘nkj’, ‘lv’ (love-penda), na ‘frsh’ (freshi) vimekuwa vikitumika zaidi, licha ya kwamba sanifu kwenye Kiswahili kama ilivyo kwa Dkt. (Daktari), S.L.P. (Sanduku la Posta), au Ukimwi (Upungufu wa Kinga Mwilini).
Je, ni kweli utitiri wa wanaokikanyaga Kiswahili kwa mtindo huo hawajui matumizi sahihi? Si kweli, bali unachoweza kukiona kwa urahisi ni ulimbukeni wa vijana, kuhisi kwamba huko ndiko kwenda na wakati. Kwa wengi wao, kuna hofu ya kuonekana ‘amechelewa’ ikiwa atachati pasi na kuchombeza kwa maneno ya ajabu.
Wasichojua walio wengi ni madhara makubwa ya mazoea yao katika utumizi mbovu wa lugha katika mawasiliano yao kwa njia ya kuchati. Kama wasemavyo Waswahili, ‘mazoea hujenga tabia’, taratibu wanapoteza uwezo wao wa kuwasiliana kwa kutumia lugha yao, Kiswahili.
Ndiyo, kama utafanyika utafiti, sina shaka kuwa kuna asilimia kubwa ya vijana wamepoteza misingi mizuri ya utumizi wa Kiswahili tangu walipojiingiza katika uhuni huo wa kuikanyaga lugha kupitia meseji zao za simu.
Labda katika kundi hilo hawatakosekana wahitimu wa elimu ya juu watakaokiri kuwa wanaendelea kuandikiwa barua za kuomba kazi. Usiulize kuhusu kuandaa ‘CV’ au ripoti za miradi kwani nazo huhitaji umahiri wa lugha katika uwasilishaji wake.
Shida inayowakuta si kwa sababu hawakufundishwa darasani, la hasha! Bila kujua, wamepoteza taratibu uwezo wao wa kuwasiliana kwa njia ya maandishi na hiyo imetokana na ‘lugha ya kuchati’ wanayoitumia siku zote.
Mwisho, vijana wanapaswa kufahamu na kutambua nafasi yao katika maandalizi ya ‘kesho’ ya jamii yao. Kama ni hivyo, basi watambue kuwa upuuzi wao katika utumizi wa lugha ni urithi utakaokuwa bomu la kuviangamiza vizazi vijavyo.