Na Yohana Paul, Geita
Ujenzi wa kiwanda cha Kuchenjulia madini ya dhahabu kinachofahamika kama Geita Gold Refinery (GGR) kinachoelezwa kuwa kikubwa na cha mfano kwa nchi za Afrika mashariki na kati umekamilika mkoani Geita huku mmiliki wake akiwa ni mtanzania ambaye ni Mwanamke kwa mkopo wa Benki ya Azania.
Akizungumzia kiwanda hicho, Mkurugenzi wa kiwanda cha GGR, Mhandisi Athuman Mfutakamba amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchenjua madini ya dhahabu kwa kiwango cha ufanisi wa asilimia 99.5 hadi 99.9 na kimejengwa kwa gharama ya dola za kimarekani (USD) 8,000,000, sawa na Sh Bilioni 20 kwa fedha za kitanzania.
Mfutakamba amesema kiwanda kina uwezo wa kusafisha dhahabu kilogramu 440 kwa siku moja, na kitakuwa na uwezo wa kununua Kilogramu 4,000 kwa mwaka za dhahabu kama malighafi kutoka kwa wachimbaji wadogo nchini na sehemu nyingine nje ya Tanzania kwa ajili ya kuziongezea ubora.
Ameeleza kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi kitaweza kuchangia kiasi cha Dola za Kimarekani kiasi cha bilioni moja kwa mwaka katika mapato ya serikali ambapo pia kimetunukiwa cheti kinachoruhusu dhahabu ya iliyochenjuliwa hapo kuweza kubadilishwa na kama fedha katika mabenki mbalimbali duniani.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi kiwandani hapo, Waziri wa madini, Dotto Biteko ametoa wito kwa watanzania hasa walio katika nafasi za uongozi serikalini na taasisi mbalimbali kubadili mitazamo yao na kuanza kuwaamini wawekezaji wazawa kwani wana uwezo wa kuleta mapinduzi kwenye sekta ya viwanda nchini.
Amesema ni wazi kwamba wakati wa mchakato wa kumpata mwekezaji wa kujenga kiwanda hicho, alipopatikana mzawa ambaye pia ni mwanamke wengi waliamini hatoweza na walijaribu kushawishi asipewe leseni lakini kilichofanyika GGR kinadhihirisha uwezo wa wawekezaji wazawa.
“Mimi mama nikwambie umetupa heshima, umetuvisha nguo, umetupa utukufu, na ninakuombea kwa Mungu akusaidie ufanikishe maono uliyonayo na jambo liweze kuisha vizuri, nataka nikuhakikishie nikiwa waziri wa madini kila aina ya msaada utakaohitaji tutakupatia,” alisema Biteko.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel alimushukuru mwekezaji kwa kuonyesha nia na kuahidi kuwatumia wataalamu wazawa na kuwafanyia mafunzo kwa vitendo yatakayowajengea uwezo watanzania kujifunza teknolojia mpya na kuweza kusimamia miradi mingine kama hiyo.
“Naomba tuendelee kuwalinda wawekezaji wanaoendelea kuja hapa, na soko hili litaleta mapinduzi makubwa mno, mapato ya serikali yatapanda,,, na nimeongea na kamati yangu ya ulinzi na usalama wote wanaohusika na usimamizi wa madini waanze kujipanga mtambo huu utafanya kazi masaa 24,” alisema